Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakari Kunenge, amemuagiza mkandarasi M/S Trinity Manufacturing Services Ltd. anaejenga mradi wa maji Kijiji cha Mjawa wilayani Kibiti kuhakikisha anakamilisha ujenzi huo ifikapo mwezi Disemba mwaka huu.
Pia amemuagiza Mkandarasi wa ujenzi wa mradi wa maji, Kijiji cha Jaribu Mpakani, Broadway Eng. Co. Ltd. kufanya kazi usiku na mchana ili kukamilisha ujenzi huo kabla ya Mwezi April, 2024.
Kunenge ametoa maagizo leo Novemba 7, 2023 akiwa kwenye ziara ya kikazi wilayani Kibiti kukagua miradi ya maendeleo na kusikiliza na kutatua kero za wananchi.
Pia amewaelekeza wakandarasi wa maji kuenda na kasi ya Serikali na Rais Samia Suluhu Hassan ambae amedhamiria kumtua mama ndoo kichwani.
Ameeleza kuwa kiu ya Serikali ni kuongeza kiwango cha upatikanaji wa maji Safi na salama mijini kwa asilimia 95 na Vijijini kwa asilimia 85 ambapo kwa mkoa wa Pwani umefikia asilimia 86 ya upatikanaji wa maji safi na salama.
Aidha, RC kunenge ametembelea mradi wa ujenzi wa shule mpya ya Sekondari Jaribu ambayo imejengwa ili kupunguza changamoto ya wanafunzi wanaotoka Mjawa kutembea umbali mrefu kufuata elimu ya Sekondari ambako ameelezwa kuwa bado kinahitajika kiasi cha shilingi milioni 210 kukamilisha ujenzi wa shule hiyo.
Mkuu huyo wa mkoa ameahidi kuzungumza na Katibu Tawala mkoa pamoja na Mkurugenzi wa halmashauri hiyo kuangalia namna ya kulitafutia ufumbuzi.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.