Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhe. Abubakar Kunenge, amekemea vikali tabia ya kutumia nyumba za ibada kwa masuala ya siasa, akisema hali hiyo inachangia kwa kiasi kikubwa kuleta mvurugano katika jamii.
Kunenge aliyasema hayo Septemba 21 katika sherehe za Maulid ya kuzaliwa kwa Mtume Muhammad (S.W.) zilizofanyika mjini Kibaha, zilizoratibiwa na Baraza la Waislamu Mkoa wa Pwani (BAKWATA).
“Ni muhimu viongozi wa dini wajiepushe na siasa ili tuendelee kuhubiri maneno ya kiimani zaidi,” alisema Kunenge.
Pia aliwataka viongozi wa dini zote kuhubiri zaidi suala la amani na kuepuka siasa, akisisitiza umuhimu wa kulinda amani ambayo imejengwa kwa muda mrefu na kusema kuwa, "tusiharibu amani kwa namna yoyote ile."
Katika hatua nyingine, Kunenge aliwahimiza wazazi kuimarisha malezi ya watoto wao ili kukabiliana na vitendo viovu vinavyosababisha mmomonyoko wa maadili katika jamii. Akizungumzia ongezeko la maadili mabaya, alisema serikali inaendelea na jitihada za kupambana na hali hii ambayo ni tishio kwa ustawi wa jamii.
Naye, Mufti wa Tanzania, Shekhe Abubakar Zubeir, alisisitiza umuhimu wa wananchi kuheshimiana, akibainisha kuwa ukosefu wa heshima ni chanzo kikubwa cha uvunjifu wa amani. Aidha, alieleza kuwa baadhi ya tabia kama kutukana viongozi ni dalili ya ukosefu wa maadili mema.
“Kiongozi yeyote lazima aheshimiwe, na ni wajibu wa kila mmoja kutunza maadili ndani ya jamii,” alisema Mufti Zubeir.
Kwa upande wake, Shekhe wa Mkoa wa Pwani, Khamis Mtupa, aliwahimiza waumini kudumisha amani iliyopo, akisema kuwa kila kiumbe kinahitaji amani na kwamba usalama unategemea uwepo wa amani.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.