Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhe. Abubakar Kunenge, ametoa shukrani zake kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, na Waziri wa Kilimo, Mhe. Hussein Bashe, kwa kuunga mkono maendeleo ya kilimo mkoani Pwani kupitia nyanja mbalimbali kama pembejeo, fedha za miradi, na zana za kilimo.
Akizungumza jana katika hafla ya uzinduzi wa kiatilifu hai cha kuangamiza wadudu waharibifu wa mazao, THURISAVE 24, iliyofanyika kwenye kiwanda cha Heaster Bioscience kilichopo Ruvu, Mhe. Kunenge alisema msaada wa serikali umeleta matokeo chanya katika sekta ya kilimo mkoani humo. Alieleza kuwa Mhe. Bashe amekuwa mstari wa mbele kusaidia mkoa huo kwa kutoa matrekta, maturubai, na kuimarisha mnyororo wa thamani wa zao la korosho.
“Uliona juhudi zetu na matokeo yanaonekana, umetusaidia kwa mambo mengi, ikiwemo matrekta, maturubai, na kuimarisha sekta nzima ya korosho. Umetusaidia sana, na mimi nakushukuru sana,” alisema Mhe. Kunenge.
Aidha, alisema matrekta yaliyopokelewa yameshaanza kutumika, na Mradi wa BBT (Building Better Tomorrow) uko katika hatua ya kuandaa udongo. Aliongeza kuwa mradi mkubwa wa kilimo cha ndizi na chikichi utakuwa mojawapo ya miradi mikubwa barani Afrika na duniani.
Mhe. Kunenge pia alimwomba Mhe. Bashe kuendelea kutoa muongozo wa namna ya kuongeza uzalishaji wa mazao kutoka mkoani Pwani ili kutimiza azma ya Mhe. Rais Samia ya kuhakikisha Tanzania inakuwa taifa la kulisha dunia, akisisitiza kwamba Pwani inaweza kuwa mfano wa mafanikio katika kilimo.
Kwa upande wake, Waziri Bashe alikipongeza kiwanda cha Heaster Bioscience kwa kubuni kiatilifu kinachotumia viumbe hai badala ya kemikali, akisema kuwa ni suluhisho rafiki kwa mazingira katika kudhibiti viwavijeshi vamizi ambao ni tishio kwa wakulima wa mahindi. Alisisitiza umuhimu wa kuendelea na tafiti zaidi katika sekta ya biochemical na bio-fertilizers kwa kushirikiana na kiwanda kikubwa cha kibaolojia ambacho kipo katika hatua za mwisho za ujenzi.
Waziri Bashe pia alimwagiza Mkurugenzi wa Mazao kuhakikisha kiatilifu hicho kinanunuliwa na kusambazwa kwa wakulima kupitia fedha zitakazotengwa kwa ajili ya viatilifu.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.