Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge ameendelea kuhamasisha wananchi kujitokeza kujiandikisha kwenye daftari la wapiga kura kwa kuendesha mbio za taratibu za kukimbia (Joging) zenye zaidi ya kilomita 5.
Mbio hizo zimefanyika Mjini Kibaha leo Oktoba 12 kuanzia ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani kupitia barabara ya Morogoro na kuelekea Soko la Loliondo na kisha kumalizia katika viwanja vya stendi ya zamani iliyopo Mailimoja Kibaha Mjini zikiwa na lengo kuhamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi kujiandikisha katika Daftari la Mpiga Kura kuelekea Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba 27 mwaka huu.
Mhe. Kunenge aliwashukuru wananchi wa Kibaha kwa kujitokeza kwa wingi na akawasihi wafanye vivyo hivyo katika zoezi la uandikishaji. Alitoa rai kwa wananchi kujiandikisha mapema na kuepuka kusubiri hadi siku za mwisho ili kuepuka msongamano katika vituo vya kujiandikisha.
“Nawashukuru sana. Kama mlivyojitokeza kwa wingi asubuhi ya leo na kwa hamasa kubwa, kila mwananchi aliyefikisha umri wa miaka 18 ajitokeze kujiandikisha kwa ajili ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba 27 mwaka huu. Zoezi la uandikishaji, ambalo Mhe. Rais amelizindua kitaifa jana, tumeanza pia jana tarehe 11. Zoezi hili halichukui muda, ni nusu dakika tu na unakuwa umemaliza,” alisema Mhe. Kunenge.
Mbali na kuhamasisha wananchi kujiandikisha, Mhe. Kunenge pia alisema mbio hizo zina faida ya kujenga afya ya mwili.
Mbio hizo ilihitimishwa katika viwanja vya Maili Moja, Stendi ya zamani ya Mabasi, ambapo wananchi walifanya mazoezi mepesi, huku wasanii mbalimbali kama Barnaba Classic na Joh Makini wakitumbuiza.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.