Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhe. Abubakari Kunenge ametoa onyo kwa wananchi wenye tabia ya kuvamia mashamba yaliyofutwa umiliki kutofanya hivyo mpaka pale Mhe. Rais atakapotoa maelekezo ya matumizi ya maeneo hayo.
Mhe. Kunenge ametoa onyo hilo aliposhiriki uzinduzi wa "Bagamoyo Ardhi Clinic" iliyofanyika katika viwanja vya Shule ya msingi Mtambani Mapinga na kuhudhuriwa na Waziri wa Ardhi Nyumba na maendeleo ya Makazi Mhe. Jery Slaa (Mb) pamoja na Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Pauline Gekul (Mb).
Akizungumza katika uzinduzi huo Mhe. Kunenge ameeleza kuwa katika mkoa huo, Kata ya Mapinga ndiyo inayoongoza kwa kuwa na migogoro mingi ya ardhi na kwamba eneo hilo la mgogoro ni changamoto kubwa kwa sababu linagusa wananchi wa ngazi ya chini.
Aidha, Mhe. Kunenge ametumia fursa hiyo kumpongeza Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo Mhe. Halima Okash kwa kufanya Kliniki hiyo yenye lengo la kukomesha Migogoro ya Ardhi na akaeleza matarajio yake kuwa Kata ya Mapinga iwe mfano wa maeneo korofi iliyofanikiwa katika utatuzi wa Migogoro ya Ardhi huku akiwaasa wananchi kutii na kuheshimu Sheria ili kila mtu apate haki yake.
Pia ameupongeza mhimimili wa Mahakama kwa kukubali kusikiliza Mashauri yaliyokaa muda mrefu ili kumaliza kesi hizo na akawataka wananchi kuheshimu maamuzi ya mahakama na maridhiano kwa wale watakaoridhiana nje ya Mahakama.
Kadhalika, Mhe. Kunenge ameelekeza wenye maeneo makubwa katika mkoa huo kujitokeza kushirikiana na Wakurugenzi wa Halmashauri kuyapanga maeneo hayo na kuwaletea maendeleo badala ya kuyaacha bila maendelezo.
Vilevile Mkuu huyo wa Mkoa ametumia nafasi hiyo kumueleza Waziri wa Ardhi kwamba Mkoa wa Pwani una maazimio nane ya Baraza la Mawaziri na utekelezaji wake unaendelea na kuwaelekeza wenye mtazamo tofauti kufuata utaratibu.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.