Mkuu wa Mkoa wa Pwani mhe Abubakari Kunenge, amepokea transforma katika mradi wa kituo cha kupoza na kupokea umeme cha Chalinze ,yenye uwezo wa megavoti 250 kwa gharama ya Bilioni 7.5.
Kuwasili kwa transforma hiyo ni muendelezo wa Mradi huo ambao kwa Sasa umefikia asilimia 53.13, unatarajiwa kukamilika mwezi Julai mwaka huu ambapo hadi kukamilika mradi mzima utagharimu Bilioni 128 fedha kutoka serikalini.
Akipokea transforma hiyo ,katika kituo hicho huku akiwa ameambatana na ujumbe kutoka Tanesco mkoa , makao makuu na Halmashauri ya Chalinze, Kunenge alisema ,ujio wa kifaa hicho unaandika historia mpya nchini kwani unakwenda kujibu changamoto ya upungufu wa umeme kwenye Maeneo mbalimbali.
Kunenge alieleza, mkoa huo umesheheni kwa viwanda, hivyo hitaji kubwa la wawekezaji ni kupata umeme wa kutosha.
"Tunashukuru Serikali, kwa jitihada za kupunguza tatizo la nishati ya umeme nchini kwa kuendeleza mradi mkubwa wa kimkakati wa bwawa la kufua umeme la Mwalimu Nyerere (stigo) litakalozalisha megawatt 2115."alieleza Kunenge.
Kwa upande wake meneja miradi Tanesco makao makuu,Didas Lyamuya alifafanua kwamba, shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), limeanza kupokea moja ya mashine umba (transforma) sita yenye uwezo wa megavoti 250 katika kituo hicho.
"Kati ya mashine umba hizi sita, mashine umba nne zitakuwa zikipokea umeme mkubwa wa kilovoti 400 utakaosafirishwa kutoka katika mradi wa bwawa la kufua umeme la Julius Nyerere (JNHPP) nakuupoza hadi kilovoti 220 na mashine umba mbili ni kwa ajili ya kuupoza umeme mkubwa kutoka kilovoti 220 hadi kilovoti 132. "
"Mashine umba hizi zina uwezo wa kusafirisha hadi megawati 800 zaumeme katika miundombinu ya umeme iliyopo sasa hivi"alieleza Lyamuya.
Hata hivyo Lyamuya alieleza kuwa, kituo hicho kilianza kujengwa mnamo mwaka 2021 na mkandarasi TBEA kutoka China na umefikia asilimia 53.13 na unatarajiwa kukamilika ifikapo tarehe 30 Julai, 2023.
Meneja wa mradi wa kituo Cha kupoza umeme Chalinze, Newton Mwakifwamba alieleza, kukamilika kwa kituo kutasaidia kufupisha njia ya kusafirisha umeme mkubwa kwani sasa
umeme mkubwa utakuwa ukisafirishwa kwenda Zuzu Dodoma ili uingizwe kwenye backbone ya
Taifa.
"Umeme mkubwa mwingine utasafirishwa kwenda Kinyerezi Dar Es Salaam na mwingine
utasafirishwa kwenda Segera Tanga na transforma hii iliyopokelewa moja ni moja ya mashine umba tano na reactors mbili zilizobakia zinatarajiwa kuwasili katika kituo hiki cha kupokea
na kupoza umeme mkubwa cha Chalinze tarehe 3, 7, na 17 ya mwezi Machi 2023."alisema Newton.
Nae Meneja Tanesco mkoa wa Pwani,Mahawa Mkaka kwa upande wake aliwataka wananchi waendelee kuvumilia tatizo la kukatikakatika kwa umeme kutokana na mabadiliko yanayofanyika kutokana ujenzi wa mradi huo.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.