Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge, amepongeza juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan katika kuleta maendeleo mkoani humo, hususan katika sekta za nishati, elimu, na maji.
Akizungumza katika mbio za Samia Marathon zilizofanyika katika viwanja vya Shule ya Msingi Mtongani, Mlandizi, Kibaha Vijijini, Kunenge alibainisha kuwa upatikanaji wa umeme vijijini umefikia asilimia 98, huku upatikanaji wa maji ukifikia asilimia 86.
Aidha, shule mpya za msingi 50 na sekondari 42 zimejengwa, pamoja na ukarabati wa mabweni na maboma.
Katika sekta ya Viwanda alisema kuwa mpaka sasa kuna Viwanda vipya 131 kati yake viwanda 78 vikubwa Vimejengwa ndani ya miaka minne.
Katika tukio hilo, Makamu Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi (CCM) Taifa, Dogo Mabrouk, alimwakilisha Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, na kusisitiza kuwa CCM inatekeleza ilani yake kwa kutatua changamoto za wananchi. Alisema Rais Samia ni kielelezo cha uchapakazi na maendeleo, hivyo Watanzania wanapaswa kumuunga mkono kwa ajili ya mafanikio zaidi.
Mbio hizo zilibeba kaulimbiu ya kuhamasisha wananchi kujitokeza kupiga kura katika uchaguzi mkuu ujao mwezi Oktoba. Mabrouk alikumbusha kuwa ingawa wengi hujiandikisha, bado kuna changamoto ya watu kushindwa kujitokeza siku ya kupiga kura, na aliwasihi wananchi kuwa sehemu ya mchakato wa uchaguzi kwa haki na kwa wingi.
Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa kupitia Wazazi mkoani Pwani, Hamoud Jumaa, alisisitiza umoja na mshikamano kuelekea uchaguzi mkuu, akibainisha kuwa umoja ndani ya chama utaleta ushindi kwa CCM. Pia, alihimiza kudumisha amani na utulivu ili kuendeleza mafanikio ya taifa.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Mkoa wa Pwani, Josian Kituka, aliwashukuru wadau wote waliofanikisha mbio za Samia Marathon, akieleza kuwa lengo kuu la mbio hizo ni kuhamasisha wananchi kujitokeza kupiga kura.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.