Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mh. Abubakar Kunenge amesisitiza ushirikiano kati ya ofisi yake na kituo cha uwekezaji Tanzania - TIC ili kufanikisha matokeo ya kukuza uchumi wa wananchi na taifa.
Kunenge ametoa msisitizo huo leo Agosti 17, 2023 alipokutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mtendaji Kituo cha uwekezaji Tanzania Gilead Teri kuhusu hali ya uwekezaji katika Mkoa wa Pwani.
Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika kwenye ofisi ya Mkuu huyo wa Mkoa mjini Kibaha, Kunenge ameelezea hali ya upatikanaji wa umeme na gesi, uboreshaji miundombinu ya barabara na mifumo ya maji kama sehemu yakuchochea uwekezaji kutokana na maeneo ya kimkakati katika mkoa huo kufuatiliwa na wawekezaji wengi wanaohitaji kutekeleza shughuli za kilimo, ujenzi wa viwanda na kuendesha biashara kwa kukuza uwekezaji walionao tayari, kuanzisha biashara mpya na kuongeza mitaji yao.
Kutokana na hali hiyo, Kunenge ameeleza kuwa ofisi yake ikifanya kazi kwa pamoja na TIC watakuwa wamefanikisha azma ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dr. Samia Suluhu Hassan ya kuwapatia wananchi maendeleo.
"Wananchi wanahitaji huduma, wapate maji, huduma za afya, huduma za elimu, umeme na mengineyo ambayo yote ni matumizi ya fedha kutoka serikalini, sasa tunahitaji kuwa na mikakati mizuri na isiyosumbufu kwa wananchi ya kuongeza mapato na uwekezaji ni njia nzuri ya kutupatia mapato hayo ili yatumike kukidhi matarajio ya wananchi," amesema Kunenge.
Amesema kuwa kwa kuongeza uwekezaji, mkoa wake utakuwa umeongeza ajira kwa wananchi, kuongeza mapato ya serikali na kuongeza upatikanaji wa fedha kupitia CSR.
Kunenge pia ameeleza namna mkoa huo unavyotekeleza mkakati wa utatuzi wa migogoro mbali mbali ikiwemo ya ardhi ili kurahisisha uwekezaji kufanyika Kwa uhakika na katika mazingira salama na akasema tayari uandaaji wa ramani maalumu kwa teckonolojia ya kisasa ya maeneo ya uwekezaji wa viwanda utakaosaidia yeyote kupata taarifa kupita simu janja (Smart phone) unakamilika na kuwa kilichobaki ni taratibu za uzinduzi.
Naye Teri amesema kuwa kufuatia jitihada na mafanikio ya mkoa wa Pwani katika uwekezaji, tayari taasisi hiyo imeanzisha ofisi ya Kanda Maalum kushughulikia uwekezaji mkoa huo ili kurahisisha utoaji wa huduma.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.