Serikali Mkoani Pwani imewataka waajiri wote kuwasajili, kuwasilisha michango ya wafanyakazi na kutoa taarifa zao za ugonjwa na ajali ili wahusika wapate huduma za fidia kwa wakati kutoka Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi nchini WCF.
Rai hiyo imetolewa leo Septemba 26, 2023 na Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge wakati akifingua mafunzo ya siku moja kwa Makamanda wa Jeshi la Polisi Tanzania, Kikosi cha Usalama barabarani kutoka Wilaya
Amesema mafunzo hayo yanalenga kuwapa uelewa kuhusu sheria ya fidia kwa Wafanyakazi (Sura ya 263) ili kufahamu mafao ya fidia yanayotolewa na WCF, taratibu za uwasilishaji madai na umuhimu wa taarifa ya Polisi katika kuchakata madai ya fidia kwa ajali zinazotokea barabarani.
“Nimetaarifiwa kuwa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi - WCF umeweka utaratibu rafiki kwa waajiri kujisajili, kuwasilisha michango ya wafanyakazi na kuwasilisha taarifa za ajali ama ugonjwa. Utaratibu huu ni kwa njia ya mtandao ambao hauhitaji mwajiri wala mfanyakazi kupoteza muda wa kutafuta au kufika ofisi za WCF ili kupata huduma,” amesema Kunenge.
Katika mafunzo hayo, Kunenge Pia ameutaka Mfuko huo kuendelea kutenda haki kwa kufuata sheria kanuni na taratibu bila kufanya upendeleo wowote au kumpunja mtu yeyote pale anapodai haki au fidia yake.
Ameongeza kuwa serikali inayo nia njema ya kufikisha huduma muhimu kwa wananchi kwa wakati na kuwa taasisi ya WCF na Jeshi la Polisi zina umuhimu mkubwa katika kuisaidia serikali kutimiza wajibu wake kama sehemu pia ya utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi CCM (Ibara ya 130) ambayo inaelekeza kuimarisha ufanisi katika hifadhi ya jamii, hususan katika kutoa fidia stahiki kwa wakati.
Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa amesisitiza WCF kuendelea kuhamasisha wafanyakazi ili waweze kutoa taarifa haraka za ajali barabarani katika vituo vya Polisi kwa madai ya kupata nyaraka ambazo ni za lazima ili waweze kuchakata madai ya ajali.
Awali, Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi, Emmanuel Humba amesema WCF ni Taasisi ya Hifadhi ya Jamii iliyoanzishwa kwa Sheria ya Fidia kwa Wafanyakazi, Sura 263 lengo likiwa ni kulipa fidia kwa mfanyakazi au wanufaika baada ya mfanyakazi kuumia, kuugua ama kufariki kutokana na kazi.
Ameongeza kuwa mfuko huo ulianza kutekeleza majukumu yake ya awali mwaka 2015 na Julai mosi 2016 ulianza rasmi kupokea madai na kulipa fidia ambapo umeendelea kutekeleza kwa ufanisi mkubwa majukumu yake yote ya msingi kama vile kulipa fidia za ajali za kikazi zinazotokea barabarani na ajali za kikazi zenye viashiria vya jinai, Sheria inataka kuwepo na taarifa za Polisi kama uthibitisho.
“Mafunzo haya ni sehemu ya utekelezaji wa ushirikiano kati ya Jeshi la Polisi na WCF na yanalenga kuwajengea uwezo watendaji wa Jeshi la Polisi, hususani Kikosi cha Usalama Barabarani, uelewa wa sheria ya fidia ili waweze kuharakisha ulipaji wa fidia zinazotokana na ajali za barabarani,” amesema Humba.
Humba ameeleza kuwa mafunzo hayo tayari yalishatolewa kwa viongozi wakuu wa jeshi la Polisi, Makamanda wa Polisi wa Mikoa na sasa ni kwa Wakuu wa Usalama Barabarani Wilaya wakianza na wa Mkoa wa Pwani na Dar es Salaam na watawafikia walioko kwenye Wilaya zingine nchi nzima.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.