Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge amewataka maofisa elimu wa Wilaya za Mkoa huo kuhakikisha vipindi vya michezo vinazingatiwa kama yalivyo masomo mengine.
Ameyasema hayo Mjini Kibaha wakati akipokea mipira 1,000 iliyokabidhiwa na Chama Cha Soka Mkoa wa Pwani (COREFA) kwa ajili ya wanafunzi kwenye shule za Wilaya zinazounda mkoa huo.
Kunenge amesema kuwa mipira hiyo ambayo imetolewa na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa Pwani (COREFA)kwa lengo la kuendeleza soka la vijana litasaidia sana kwa wachezaji wanao ibukia mashuleni.
Amesema kuwa michezo ni ajira na wanamshukuru Rais Dk Samia Suluhu Hassan kuwekeza kwenye michezo ambapo matunda yanaonekana kwani soka limekuwa na hamasa imekuwa kubwa.
Kwa upande wake mwenyekiti wa COREFA Robert Munis amesema kuwa mipira hiyo iwe chachu kwa wachezaji wachanga ili waje kuwa wachezaji wazuri watakaoiletea nchi sifa.
Munis amesema ili vipaji viweze kuonekana lazima kuwe na msingi wa wachezaji kuanzia chini ili wakue kwenye mazingira ya uchezaji kwa kuwa na vifaa kama vile mipira.
Naye Katibu Tawala wa Mkoa huo Rashid Mchatta akiwakabidhi mipira maofisa elimu wa Wilaya amesema kuwa mipira hiyo imekuja wakati mwafaka kwani itasaidia kukuza michezo mashuleni.
Mchatta amesema kuwa mipira hiyo pia itasaidia kwa ajili ya wachezaji wanafunzi wakati wakishiriki michezo kwa shule za msingi (UMITASHUMTA) na sekondari (UMISSETA).
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.