Mkuu wa mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge amewaelekeza watumishi wa umma kujituma pasipo kuchoka ili kufanikisha azma ya Serikali kuwaletea wananchi maendeleo.
Kunenge ametoa maelekezo hayo kwa nyakati tofauti katika halmashauri za Kisarawe, Rufiji na Kibiti wakati alipozitembelea na kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika maeneo hayo ambayo itakaguliwa, kuwekewa jiwe la msingi, kufunguliwa au kuzinduliwa na Mwenge wa Uhuru kwa mwaka 2025.
"Mimi kwenye nafasi yangu na ili tumpe heshima Mhe. Rais aliyeelekeza Mwenge wa Uhuru uzinduliwe Mkoani kwetu (Pwani), kama kuna jambo litahitaji uwepo wangu nisilale, sintalala ili kuhakikisha kuwa mambo ya uzinduzi yanaenda sawa sawa," alisema.
Akiwa Kisarawe, Kunenge aliwasisitiza watumishi kujituma zaidi akiwahimiza kuwa ili wafanye vizuri katika utendaji wao ni lazima wawe na moyo wa kutaka kufanya hivyo.
"Mwenyezi Mungu amekupa uwezo na akili, kwanini ushindwe, tatizo ninaloliona ni kuwa watu wanataka kufanyiwa kazi zao," alibainisha.
Akitahadharisha juu ya utendaji usioridhisha kwa baadhi ya watumishi, Mkuu huyo wa mkoa alieleza kuwa kuna mambo ya kubembelezana lakini kuna mambo mengine sio ya kubembelezana na akatoa mfano wa usimamizi hafifu katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo akihoji kwa kutoa mfano kuwa inawezaje kutokea mlango usifunge wakati wataalam wenye ujuzi wapo na mifumo ya ufuatiliaji nayo ikiwepo.
Hata hivyo Kunenge ambaye anaendelea na ziara yake hiyo inayolenga kuzifikia Halmashauri zote za Mkoa huo aliwapongeza watalamu kwenye maeneo yao kwa kujituma akisema "ninaamini tunayo timu nzuri, tukijipanga tunaweza kufanya vizuri
Kila mmoja afanye kazi na ajitume."
Mbio za Mwenge wa Uhuru zinatarajiwa kuzinduliwa Mkoani Pwani April 2, 2025 kwenye viwanja vya Shirika la Elimu Kibaha na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali na wananchi kwa makundi tofauti.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.