MKUU wa Mkoa wa Pwani Abubakari Kunenge, amewataka wataalamu wa Mkoa huo, kutumia Matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022, kupanga mipango vizuri ili kutekeleza miradi mbalimbali kulingana na mahitaji ya wananchi.
RC Kunenge ametoa kauli hiyo leo Mei 31, 2023 akizungumza katika mafunzo ya Matumizi ya Matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi kwa Kamati ya Sensa Mkoa, Sekretarieti ya Mkoa na Viongozi wa Ngazi ya Mkoa wa Pwani yaliyofanyika kwenye ukumbi wa Chuo cha Kimataifa cha Mwalimu Nyerere mjini Kibaha.
"Tuna mipango mbalimbali, hivyo tuchukue data tulizopata kuziweke katika uhalisia wa mipango yetu," amesema RC Kunenge na kuongeza,
"Nitumie fursa hii kuwaagiza wataalamu wangu kutumia takwimu hizi kuangalia ni wapi tuwekeze nguvu hivyo tuanze kufanya uthibitishaji wa mipango yetu,.
Rc Kunenge ameahidi kufanyia kazi takwimu hizo na kusisitiza kwamba zitawapa dira na mwelekeo mzuri katika kuwahudumia wananchi wa mkoa wa Pwani.
Kamisaa wa Sensa ya Watu na Makazi Tanzania Bara Anne Makinda amewashukuru watanzania pamoja na timu yake kufanikisha jukumu la utekelezaji wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022.
Naye Kamisaa wa Sensa Tanzania Zanzibar Balozi Mohamed Haji Hamza amesema jukumu la sasa kwa viongozi ambao wamepata mafunzo hayo ni kusaidia kusambaza matokeo hayo na kuwafikia wananchi wote.
Sambamba na hilo amesema ni kuyaelewa matokeo hayo na namna ya kuyatumia kwa ajili ya mipango ya maendeleo, kwamba lengo ni kujenga jamii yenye kuelewa takwimu za Sensa na kuzitumiwa kwa mipango yao ya maendeleo.
Kwa mujibu wa Matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022 Mkoa wa Pwani una jumla ya watu 2,024,947 ambapo kati ya hao Wanaume ni 998,616 huku Wanawake wakiwa ni 1,026,331.
Idadi ya watu wenye umri wa kufanya kazi (15-64) ni milioni 1,175,494 sawa na asilimia 58.1, idadi ya wazee wenye umri wa miaka 64 na kuendelea ni 128,432 sawa na asilimia 6.3.
kuhusu idadi ya watoto na vijana ni kwamba kwa vijana wa miaka kati ya 15-25 ni 738,763 sawa na asilimia 36.5 huku watoto wa kati ya miaka 0-14 wakiwa ni 761,525 sawa na asilimia 37.6.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.