Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhe. Abubakar Kunenge leo mei 2, 2023 ametembelea, kukagua, kusikiliza na kutatua kero za wasafiri kwenye Kituo cha Mabasi cha kibaha (Kibaha Bus Terminal).
Akiwa kwenye ukaguzi huo amesikiliza kero za Wananchi waliokuwa katika eneo hilo na kuzitatua huku akitoa maelekezo ya maboresho kutokanana na malalamiko ya wananchi kama yalivyofikishwa kwake.
Baadhi ya kero zilizowasilishwa kwake ni pamoja na kuchelewa kufika kwa mabasi ya Mwendekasi kituoni hapo ambayo yanafanya safari zake Kati ya Kibaha na Dar es Salaam, uduni wa mabanda ya kujikingia jua na mvua yaliyojengwa kwenye eneo hilo pamoja na kujaa maji kwa baadhi ya maeneo ya kituo hicho cha magari.
"Yaani tatizo lipo hapo hapo na tulipowaoneni tukasema leo kilio chetu kimekwisha, na ndio maana unaona nimekaa kule nikawafuateni fasta, yaani hicho ni kilio kikubwa saana," alisema Ashura Juma mkazi wa Kibaha, Picha ya ndege aliyekuwa kwenye kituo hicho cha magari.
Akitolea maelekezo ya utatuzi wa changamoto hizo, Mhe. Kunenge alisema kuwa kuhusu suala la magari ya mwendokasi atafuatilia kwa karibu kwa kiongozi msimamizi wa kampuni hiyo ingawa alipowasiliana kwa simu na kuweka bayana kuwa wananchi wamelalamika kuwa kwa sasa huduma hiyo hairidhishi na kiongozi huyo kuahidi kuongeza Mabasi hayo na Viongozi wa DART kutembelea eneo hilo, pia alielekeza uongozi wa halmashauri ya Kibaha kufanya marekebisho kwenye mapungufu yaliyobainishwa kupitia hoja za wananchi (wasafiri) katika kituo hicho haraka iwezekanavyo.
Akijibu kero za Wananchi Kunenge alisema "nia ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na wasaidizi wake ni kutatua kero za Wananchi na kuwarahisishia utoaji wa Huduma."
Kuhusu eneo la kuegesha magari kuharibika na kujaa maji mabonde kwenye Kituo hicho ameagiza wataalam wa Halmshauri kushirikiana na TANROADS na TARURA kufanya matengenezo ya maeneo yaliyoharibika na akamtaka Mkurugenzi wa Mji kuangalia kuelekeza wataalam wake kufungua lango la kutokea abiria na kurekebisha mabanda ya abiria (vikingia mvua na jua) na kufanya maboresho.
Awali, Mhe. Kunenge alikagua na kuridhishwa na ujenzi wa barabara ya viuatilifu.
Pia alitembelea na kukagua maendeo ya ujenzi wa Kongani ya KAMAKA ambayo tayari uzio wenye urefu wa kilomita tisa, barabara za ndani, kituo cha zimamoto na cha Polisi vyenye thamani ya sh. Bilioni 23.3 vimekamilika.
Ziara hiyo ya Mhe. Kunenge ni sehemu ya mpango wake wa kuadhimisha miaka 59 ya Muungano kwa kukagua miradi kwa kila halmashauri katika Mkoa huo.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.