Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakari Kunenge ametoa muda wa mwezi mmoja kwa wananchi waliovamia shamba la Wizara ya Mifugo na Uvuvi lililopo katika Halmashauri ya Mji wa Kibaha kuhakikisha wanalipa fedha kwa haraka kwa ajili ya kupimiwa maeneo hayo ili waweze kumiliki kisheria.
Kunenge alitoa agizo hilo leo Februari 2, 2023 katika mkutano wake na wananchi wa maeneo ya Lumumba, Mkombozi na Kidimu ambayo kwa pamoja yanaunda Kata ya Pangani ambako alifika kutoa msimamo wa Serikali kuhusu wavamizi hao.
Alisema shamba hilo ambalo ni maarufu kwa jina la "Mitamba" linamilikiwa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi likiwa na ukubwa wa hekta 4000 lakini wananchi hao walilivamia na kuanza kujenga bila kufuata sheria.
Alifafanua kuwa shamba la "Mitamba" lilianza miaka ya 1982 na 1983 likiwa chini ya Wizara ya Mifugo kwa lengo la kutoa mafunzo na uzalishaji wa Mitamba lakini wakati linaanzishwa kulikuwa na wakazi 1,557 ambao walilipwa fidia yenye thamani ya Sh. milioni 20.
Alieleza kuwa baada ya kulipa fidia hizo kukajitokeza uvamizi wa watu kujenga na wengine kufanya maendeleo bila ya kufuata sheria, kwa kuwajali wananchi wake, uongozi wa Serikali Wilaya na Mkoa ukaomba ridhaa ya Wizara husika ili wananchi hao waweze kupewa eneo hilo.
Ameongeza kuwa kutokana na hali hiyo, Wizara kupitia Katibu Mkuu aliandika barua ya kuridhia kutoa eneo la ukubwa wa hekta 2,963 na kulikabidhi katika Halmashauri ya Mji wa Kibaha kwa ajili ya makazi na mipango mingine ya maendeleo.
Amesema kuwa baada ya Wizara kutoa eneo hilo na kulikabidhi katika Halmashauri ya Mji wa Kibaha kwa sasa Wizara imebakiwa na eneo lenye ukubwa wa hekta 1037 Kitalu namba 34 ambalo halitakiwi kuguswa na mtu yeyote na kwamba wanaohusika na maamuzi ya kulipa gharama ni wale waliokuwa ndani ya eneo la Hekta 2,963 lililotolewa na Wizara.
"Machi 7, 2012, Wizara ilikabidhi hekta 2,963 kwa Halmashauri na sio kwa mtu mwingine na nyinyi mlivamia tu lakini Serikali imekaa na kuona kunahitaji la kuwasaidia wananchi wake lakini mnatakiwa kulipa gharama ili muweze kumilikishwa kisheria," alisema Kunenge na akaongeza kuwa kisheria wananchi hao walitakiwa kulipa kulingana na bei ya soko lililopo hivi Sasa lakini kutokana na huruma ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kiwango hicho kimeshuka kutoka mita ya mraba 6000 mpaka 1500 na kila mwananchi atapewa Mita za mraba 2500 kwa ajili ya makazi.
"Fedha hizo zinatakiwa kulipwa katika kipindi cha mwezi mmoja na anayemaliza anapewa hati miliki yake na kwa yule ambaye atashindwa kufuata maelekezo hayo ataondolewa na kiwanja chake Kitapewa mtu mwingine, mtambue kuwa Rais Samia amekuwa na huruma kwa wananchi wake ndio maana hata bei mliotakiwa kulipa imeshuka ili kuwasaidia watu wachini na wale wasiojiweza kabisa watasaidiwa kupitia mpango wa TASAF," alisema Kunenge.
Mkuu huyo wa mkoa alitoa ufafanuzi kuwa kwa wale ambao watahitaji eneo kubwa zaidi watapaswa kununua kwa bei ya soko ambayo ni Sh.6000 kwa kuwa mahitaji yao ni zaidi ya makazi huku akiwashauri Wananchi hao kutumia fursa hiyo kikamilifu.
Alionya kuwa asitokee mtu wa kuwadanganya kuacha kulipa viwango vilivyopangwa na Serikali kwa kuwa watakuwa wanapoteza muda na kusema asiyetaka kulipa aondoke mwenyewe.
Pia aliongeza kuwa pamoja na hayo, bado ataendelea kufanya oparesheni ya kuwakamata wale wote waliowatapeli wananchi kwa kuwauzia maeneo kinyume na utaratibu.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.