Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhe. Abubakar Kunenge amewataka wajumbe wa baraza la Ardhi wilaya ya Bagamoyo kufanya kazi kwa weledi bila kumuogopa mtu kwani hakuna aliye juu ya sheria.
Aidha amewataka kusimamia maadili katika utendaji wao wa kazi kwa kuondoa migogoro ya ardhi kwa wakati, kuondoa ugumu ambao unaweza kutokea endapo mashauri yatachelewa.
Mhe. Kunenge ameyasema hayo leo April 11, 2022 mjini Bagamoyo alipokuwa akiwaapisha wajumbe wa baraza la ardhi la Wilaya hiyo, Amesema katika utawala wa sheria hakuna aliye juu ya sheria hivyo wajumbe walioapishwa wanatakiwa kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia ufahamu, ujuzi na utaalamu na kuishi kulingana na majukumu yao.
" Mimi sitawauliza juu ya utendaji wenu nitajua ufanisi wenu kwa kuangalia ni kiwango gani mtatatua changamoto kwa jamii inayowazunguka na niwaambie hatutarajii tuwe na watu ambao hawatakuwa msaada. Tukiona hamna msaada tutawabadilisha" alisema Kunenge.
Kunenga amesema atasikitika endapo maamuzi yanayotolewa na baraza hilo asilimia kubwa yakaonekana ni batili.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo Zainabu Abdallah amempongeza Mkuu wa Mkoa kwa kuwaapisha wajumbe hao ambapo amesema kukosekana kwa baraza hilo ilikuwa kero kwa wananchi ambao walikuwa wanalazimika kwenda kibaha kufuatilia mashauri yao.
Mwenyekiti wa Baraza la Ardhi na nyumba wilaya ya Kibaha Sara Mbuga ambaye alimwakilisha Msajili wa Mabaraza ya ardhi mikoa ya Pwani na Dar es salam amewasihi wajumbe walioapishwa kufanya kazi kwa uadilifu.
Kati ya Wilaya saba za Mkoa wa Pwani tayari wilaya tano zina Mabaraza ya Ardhi na Nyumba.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.