Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhe. Abubakar Kunenge , amewakaribisha wananchi pamoja na wafanyabiashara wakubwa na wa kati kushiriki kwa wingi katika Maonesho ya Nne ya Biashara na Uwekezaji yanayofanyika katika viwanja vya Mailimoja, Kibaha Mjini. Maonesho hayo yaliyanza Disemba 16 na yanatarajiwa kufikia kilele chake Desemba 20, 2024. Ufunguzi rasmi wa maonesho hayo utafanyika Desemba 17, ambapo mgeni rasmi atakuwa Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Suleiman Jafo (Mb).
Akizungumza na waandishi wa habari disemba 16,2024, Kunenge alisisitiza umuhimu wa maonesho hayo katika kukuza uchumi wa Mkoa wa Pwani na kufungua fursa mbalimbali kwa wafanyabiashara, wawekezaji, na wajasiriamali. Alieleza kuwa maonesho hayo ni sehemu ya jitihada za Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, za kukuza sekta ya biashara na uwekezaji nchini. Mkoa wa Pwani, kwa kushirikiana na serikali kuu, umeamua kutekeleza juhudi hizo kwa vitendo kupitia maonesho haya.
Alibainisha kuwa lengo kuu la maonesho hayo ni kutangaza fursa za uwekezaji, kufungua masoko mapya, na kutoa jukwaa la kuonyesha bidhaa zinazozalishwa mkoani Pwani. Aidha, alieleza kuwa maonesho hayo yanatarajiwa kushirikisha washiriki 550, wakiwemo wafanyabiashara wakubwa, wa kati, taasisi za umma, na sekta binafsi.
Katika hatua nyingine alielezea mafanikio makubwa yaliyofikiwa na Mkoa wa Pwani chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, akisema kuwa tangu mwaka 2021, mkoa huo umefanikiwa kuongeza viwanda vikubwa 78 na kufikia jumla ya viwanda 1,553. “Tunaendelea kunufaika na mazingira bora ya uwekezaji yaliyoimarishwa na serikali inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan. Maonesho haya ni sehemu ya juhudi zetu za kutekeleza dira ya maendeleo ya viwanda nchini,” alisisitiza Kunenge.
Aidha, Mhe. Kunenge alifafanua kuwa maonesho hayo yataambatana na Kongamano la Uwekezaji litakalofanyika Desemba 18, 2024, katika Chuo cha Uongozi cha Mwalimu Nyerere, Kibaha kwa Mfipa. Kongamano hilo litatumika kama jukwaa muhimu la mijadala juu ya maendeleo ya biashara na uwekezaji mkoani Pwani na nchini kwa ujumla.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.