Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhe Abubakar Kunenge amezindua Mradi wa kilimo cha Pamba na kupokea matrekta na pikipiki zitazotumika kwenye mradi huo Wilayani Rufiji utakaotekelezwa na Kampuni ya "Rufiji Cotton Ltd.
Akizungumza na Wanachi wa chumbi kwenye hafla hiyo leo Januari 13, 2024 , Mhe Kunenge amewapongeza wawekezaji hao kutoka India kwa uwekezaji huo akisema hana shaka na mwekezaji huyo kwa sababu ni mzoefu kwenye sekta ya Pamba.
Ameeleza kuwa Serikali ipo tayari kumpa ushirikiano mwekezaji na akamtaka atekeleze yote aliyoahidi na kuwa kupitia uwekezaji huo vijana watapata ajira, ujuzi na kodi kwa serikali.
"Kilimo ndio kipaumbele kwa Mkoa wa Pwani lakini bado hakijafanya vizuri, hivyo nnawapongeza wakazi wa Chumbi kwa kuwezesha uwekezaji huu na pia nnaipongeza Wilaya ya Rufiji kwa kuendelea kuwapokea wawekezaji, kwa sasa wilaya hii ina wawekezaji wakubwa wa Kilimo cha Sukari na sasa Kilimo cha Pamba na niwaase kuzitumia fursa hizi mlizopata.
Kwenye uzinduzi huo, Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Pamba Bw. Wille Mtunga ameeleza kuwa uzinduzi wa mradi huo ni matokeo ya ziara ya Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan nchini India. Ameeleza kuwa wataalam wa Bodi hiyo wamepita katika vijiji 24 wilayani Rufiji kufundisha juu ya kilimo bora cha pamba na kuwa ili kuwa na kilimo bora, wameleta timu ya ushindi ambao ni maafisa ugani 24 watakao hudumu kwenye vijiji hivyo 24 na kuwa mpaka sasa wamesajili wakulima wenye jumla ya ekari 3012 wilayani humo na kafafanua kuwa ifikapo Jumatatu Januari 15, 2024 watapeleka mbegu za pamba, viwatilifu, mabomba ya kupulizia mazao na vyote vitagawiwa kwa wakulima bila malipo.
Kwa upande wake Balozi wa zao la Pamba nchini Mhe. Aggrey Mwanri ametuma salaam kwa Rais Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan za pongezi kwa kuvutia uwekezaji katika sekta ya Pamba. Kazi yangu kama balozi ni kufanya pamba ipendeke kwa wananchi wote, tumechukua takwimu za wananchi wote wa Rufiji waliotayari kulima Pamba kwani kilo zinazozalishwa wilayani Rufiji ni laki moja na kiwanda kitakachojengwa kitahitaji kilo laki tano kwahiyo Halmshauri hii ikilima pamba vizuri itapata ruzuku," amefafanua Mwanri.
Balozi huyo wa Pamba amehamasisha vijana wote kulima zao hilo na akawataka maafisa ugani 24 walioajiriwa kuhakikisha wanafanya kazi iliyokusudiwa.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Kiwanda cha "Rufiji Cotton Ltd." Bw Hassan Kinje ameeleza kuwa wamkwenda kuwekeza kwenye kilimo cha Pamba Rufiji kwa sababu ya Mazingira mazuri ya uwekezaji na akabainisha kuwa kampuni hiyo itatoa uwezeshaji wa huduma bure ya matrekta kwa ajili ya kilimo.
Aidha ameeleza kuwa wameajiri maafisa ugani 24 na kutoa pikipiki ambazo zitatumika kutoa elimu kwa wakulima na kwamba wanategemea kujenga kiwanda cha kuchambua Pamba na kiwanda cha nguo na akapongeza ushirikiano mkubwa walioupata kutoka kwa uongozi wa Mkoa katika kufanikisha uwekezaji huo.
Diwani kata ya Chumbi Mhe. Ally Athuman Nguyu amepongeza Wananchi kujitolea ekari 6000 kwa ajili ya kilimo cha Pamba na ujenzi wa kiwanda cha kuchakata pamba na akahamasisha wananchi kulima pamba kwa wingi kwa kuwa mwekezaji anahitaji pamba nyingi zaidi hivyo wananchi wote walime ili kuweza kulisha kiwanda hicho.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.