Mkuu wa mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge amezielekeza Halmashauri zote za mkoa huo kuandaa mikakati thabiti itakayoziwezesha kuongeza ukusanyaji mapato ili kuisaidia serikali kutoa huduma bora kwa wananchi wake.
Kunenge ameyasema oa hayo leo Agosti 15, 2023 kwenye kikao kazi maalum kilichofanyika Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha cha kuandaa mpango mkakati wa ukusanyaji mapato kwa kipindi cha miaka mitano mkoani humo.
Amesema mpango huo utakuwa ni dira ambayo utaisaidia mkoa wa Pwani kuongeza ukusanyaji wa mapato kutoka kwenye vyanzo mbalimbali ikiwemo sekta ya viwanda, uvuvi, mifugo, kilimo na uchumi wa bluu.
“Ni hatua muhimu sana kwa mkoa wetu katika kuhakikisha tunawahudumia wananchi kupitia rasilimali zetu za ndani, tunahitaji tukusanye mapato katika kila sekta lakini kwa utaratibu mzuri ambao hautawaumiza wananchi wetu, “ amesema Kunenge.
Ameongeza kuwa mkoa wa Pwani umekuwa wa kwanza kujengewa uwezo na Serikali ya watu wa Ujerumani GIZ katika kufanikisha mpango bora wa ukusanyaji mapato na kwamba watahakikisha mkoa huo unakuwa kinara wa mapato nchini.
Aidha, Kunenge amewashauri wakuu wa mikoa wengine nchini kujifunza mbinu za kisayansi za kukusanya na kuongeza mapato na kwamba ofisi yake ipo tayari kutoa uzoefu wake ili kwa pamoja waisaidie serikali kupata fedha za kuwahudumia wananchi.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Nickson Simon amesema mpango huo wa miaka mitano utasaidia kuongeza ukusanyaji mapato kutoka sh. bilioni moja hadi bilioni 20.
Amesema miongoni mwa vyanzo wanavyovikusudia ni bandari kavu ya Kwala, mradi wa ujenzi wa nyumba na viwanja vya michezo.
“Tunaamini mbinu hizi za kisayansi zitatusaidia sisi Kibaha kuongeza ukusanyaji wa mapato na tupo tayari kulisimamia hili kwani uwezo wa kufanya hivyo tunao kwa sababu tuna rasilimali za kutosha.
Naye Mtaalam Msimamizi wa Fedha za Umma kutoka Serikali ya Watu wa Ujerumani GIZ nchini Tanzania, Eriko Amon amesema kuwa mpango huo utasaidia kuweka utaratibu wa kuwatambua wafanyabiashara, kuchambua maeneo yanayosababisha fedha kukosekana ili kuongeza ukusanyaji wa mapato.
Katika kikao hicho, Nsajigwa George aliyemuwakilisha Katibu Tawala mkoa wa Pwani amesema kuwa mpango huo ni utekelezaji wa maagizo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan sambamba na dira ya maendeleo ya mkoa huo.
Amesema mkakati huo wa utekelezaji ni matokeo ya jitihada zinazofanywa na viongozi wa mkoa huo katika kuisaidia serikali kupata fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya wananchi.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.