Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge, amesema yeye kwa kushirikiana na viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo, watafanya kazi maalum kuhakikisha wanatumia historia ya Mji wa Bagamoyo na bahari ya Hindi kuongeza mapato.
Kunenge ameyasema hayo leo Juni 21, 2023 katika kikao cha Baraza la halmashauri maalum la kupitia hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka wa fedha 2022/2023.
Amesema fursa zilizopo wilayani Bagamoyo hazitangazwi ipasavyo hivyo wanapaswa kufanya kazi maalum kuhakikisha wanaongeza mapato kupitia historia na ukongwe wa mji huo pamoja na uwepo wa bahari ya Hindi.
“Tunapaswa kufanya kazi maalum hapa kuongeza mapato, haiwezekani tuna mji mkongwe na wa kihistoria lakini kasi ya ukusanyaji mapato ni ndogo vile vile bahari yetu ambayo kwa sehemu kubwa ipo hapa Bagamoyo tuumize vichwa vyetu kuhakikisha tunabuni fursa zinazopatikana mule majini,” amesema Kunenge.
Kunenge pia amewataka viongozi wa Wilaya hiyo kuainisha maeneo yote yasiyokuwa na migogoro ya ardhi kwa ajili ya shughuli za Utalii na Uwekezaji kama sehemu ya kukuza uchumi wa eneo hilo.
Akiwa katika halmashauri ya Wilaya ya Chalinze Kunenge, amesema licha ya Halmashuari hiyo iliyopo Wilaya ya Bagamoyo kupata hati safi baada ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali - CAG kufunga hoja 19 kati ya 32 kwa mwaka 2022/2023, viongozi wanapaswa kubuni vyanzo vingine ili kuongeza mapato.
Amesema ni muhimu kwa viongozi wa Halmashauri hiyo kuumiza vichwa kubuni zaidi vyanzo vya mapato ambavyo vitasaidia kuipaisha kimapato na kuisaidia serikali kutimiza majukumu yake yanayoondoa kero kwa wananchi.
“Halmashauri ya Chalinze kupata hati safi sio jambo la kushangaza sana, sasa tujikite pia kwenye kubuni na kutafuta vyanzo vingine vya mapato ili uchumi wetu upae na tuweze kutekeleza majukumu yetu ipasavyo kwani tuna eneo kubwa la ardhi, tulitumie vizuri na tuandae mazingira mazuri ya kuwavutia wawekezaji,” amesema Kunenge.
Hata hivyo, Mkuu huyo wa Mkoa amezipongeza halmashauri hizo kwa kupata hati safi na akawahimiza kuendelea kupata majibu ya zile zilizobakia ili nazo zifutwe.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.