Mkuu wa mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge, ameeleza kuridhishwa na namna bonde la Mto Ruvu limelindwa kwa kuhakikisha hakuna uharibifu katika vyanzo vya maji vinavyoweza kusababishwa na shughuli za kibinadamu kama vile ufugaji na kilimo.
Kunenge ametoa kauli hiyo leo Novemba 4, 2023 kwenye ziara ya kukagua na kuangalia hali ya utunzaji wa bonde la Ruvu ambalo lina vituo viwili vya kuzalisha maji, Ruvu juu na chini mkoani Pwani.
Katika ziara hiyo, RC Kunenge aliambatana na Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Shaka Hamdu Shaka ambaye alimwakilisha Mkuu wa mkoa wa Morogoro Adam Malima, timu ya wataalam kutoka ofisi ya bonde la otiWami - Ruvu, Mamlaka ya Maji safi na Salama Dar es Salaam DAWASA, na timu ya waandishi wa habari ambao wamefika na kujionea kazi nzuri iliyofanywa ya utunzaji wa bonde hilo.
Amesema ziara hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa jukumu la kusimamia bonde hilo ili kuwa na kiwango kikubwa cha maji ambacho kitasaidia upatikanaji wa uhakika wa maji kwa wananchi wa mikoa ya Pwani na Dar es Salaam pamoja na usafi wa kutoa taka kwenye bonde hilo ili maji yanayopatikana yawe safi na salama.
“Baada ya kubaini bonde hili lina upungufu mkubwa wa maji kwa miaka ya nyuma, tulikubaliana sisi wakuu wa mikoa ya Morogoro, Pwani na Dar es Salaam kuweka mikakati itakayowezesha maji kupatikana kwa wingi, mikakati hiyo ni pamoja na kuhamasisha zoezi la upandaji miti kuzunguka bonde hilo, kuzuia shughuli za kibinadamu ikiwemo uchepushaji wa maji kwa ajili ya kilimo na ufugaji iliyokuwa inafanywa na baadhi ya wananchi,” amesema Kunenge.
Ameongeza kuwa baada ya kazi hiyo ambayo iliwahusisha wataalam wa bonde na DAWASA, muitikio wa utunzaji umekuwa mzuri kwani shughuli za uchafuzi wa mazingira zimepungua.
Katika hatua nyingine Kunenge amewataka wananchi kuchukua tahadhari juu ya mvua zinazoendelea kunyesha kama vile kuhama kwenye mabonde na maeneo yaliyo jirani na mito ili kuwa salama dhidi ya mafuriko yanayoweza kutokea.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa mkoa wa Morogoro, Adam Malima, Mkuu wa wilaya ya Kilosa, Shaka Hamdu Shaka, amesema wanatekeleza maagizo ya Rais wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan kuhusu utunzaji wa bonde la Wami - Ruvu ambalo mwaka 2022 lilikuwa na uhaba wa maji.
Amesema kwa pamoja viongozi wa mikoa mitatu inayonufaika na bonde hilo wataendelea kufanya ukaguzi wa mara kwa mara ili kudhibiti uharibifu wa mazingira.
Mkurugenzi wa Bonde la Wami - Ruvu, Elibariki amesema mvua za vuli zinazoendelea kunyesha mwaka huu zimesaidia kuongeza maji katika bonde hilo kutoka asilimia 29 ya mwaka jana na kufikia 69.
Amesema hali hiyo inatokana na utunzaji wa mazingira katila vyanzo vya mito inayotiririsha maji yake katika bonde hilo ambalo safu zake zinaanzia kwenye milima ya Uluguru.
Ameongeza kuwa kwa sasa wana uhakika wa maji ya kusambaza kwa wananchi wa mikoa ya Pwani na Dar es Salaam na kwamba Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini TMA imewahakikishia kutakuwa na mvua nyingi ambazo zitasaidia kuongeza wingi wa maji.
S
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.