Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhe. Abubakar Kunenge, amemuagiza Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani, Pili Mnyema, kwa kushirikiana na Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Nickson Simon, kuhakikisha hatua za kisheria zinachukuliwa dhidi ya viongozi wote waliobainika kuhusika na kusababisha migogoro ya ardhi wilayani Kibaha.
Migogoro hiyo inahusisha mmiliki binafsi, Tariq Saleh Ahmed, Kampuni ya Bathawab Investment Ltd, Kampuni ya Transcontinental Forwarders Limited pamoja na baadhi ya wananchi wa maeneo ya Lupunga na Chekeleni.
Aidha, Kunenge ametoa onyo kali kwa viongozi wa Serikali za Mitaa dhidi ya kujihusisha na uuzaji wa ardhi, huku akizielekeza halmashauri zote za Mkoa wa Pwani kusimamia kikamilifu masuala ya ujenzi kwa kuhakikisha vibali vinapatikana kabla ya kuanza ujenzi, ili kuepusha migogoro isiyo ya lazima.
Vilevile, amewaelekeza wawekezaji kuendelea na shughuli zao za uwekezaji baada ya kuthibitishwa rasmi kuwa wao ni wamiliki halali wa maeneo hayo.
Maelekezo hayo yalitolewa Desemba 17, 2025, wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika katika eneo la Kikongo, Wilaya ya Kibaha, ambapo Mhe. Kunenge alikuwa akiwasilisha taarifa ya migogoro ya ardhi iliyoshughulikiwa na timu ya wataalamu kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
Timu hiyo iliundwa kufuatia Ziara ya Kliniki ya Ardhi iliyofanywa na aliyekuwa Waziri wa wizara hiyo, Mhe. Jerry Silaa, mkoani Pwani Julai 2–3, 2024.
Akizungumza katika mkutano huo, Mhe. Kunenge alisema
“Kwa kuzingatia maelekezo ya Mhe. Waziri, nimemuelekeza Katibu Tawala wa Mkoa pamoja na Mkuu wa Wilaya kuhakikisha viongozi wote waliosababisha mgogoro huu wanafuatiliwa na kuchukuliwa hatua za kisheria.”
Aliongeza kuwa viongozi wa Serikali za Mitaa hawapaswi kuhusika katika uuzaji wa ardhi, na halmashauri zote zihakikishe zinasimamia ipasavyo utoaji wa vibali vya ujenzi ili kuzuia migogoro kama hiyo kujirudia.
Akisoma taarifa ya migogoro hiyo, Katibu Tawala Msaidizi Miundombinu kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhandisi Felix Nlalio alisema mgogoro mmoja unahusu Shamba Na. 9 (Lupunga Farm Ltd) kati ya Bw. Tariq Saleh Ahmed na baadhi ya wananchi wa Kitongoji cha Lupunga.
Alisema shamba hilo lenye ukubwa wa ekari 850, lililopo Kata ya Kikongo, Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha, liligawanywa kuwa Shamba Na. 9/1 na 9/2.
Mhandisi Felix aliongeza kuwa mgogoro mwingine unahusu Shamba Na. 30/1 Chekeleni/Lupunga lenye ukubwa wa hekta 1,082.4 na Shamba Na. 30/2 lenye ukubwa wa hekta 737.6, kati ya Kampuni ya Transcontinental Forwarders Limited na baadhi ya wananchi wa Chekeleni na Lupunga.
Alifafanua kuwa kulikuwepo na malalamiko ya mara kwa mara kuhusu madai ya fidia, lakini baada ya uchunguzi wa kina uliohusisha mapitio ya nyaraka na mahojiano na pande zote husika, timu ya Wizara imethibitisha kuwa Kampuni ya Transcontinental Forwarders Limited pamoja na Bw. Tariq Saleh Ahmed ndio wamiliki halali wa mashamba hayo.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.