Mkuu wa mkoa wa Pwani Abubakari Kunenge, amesema Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan,imeitendea haki Wakala wa barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kwa kutenga kiasi cha sh. Bilioni 44.65 kwa mwaka wa fedha 2021/2022 za utekelezaji wa miradi.
Kunenge aliyasema hayo wakati alipokagua miradi ya barabara mbali mbali za Viuatilifu - TAMCO - Mapinga iliyo chini ya TANROADS, barabara ya kuelekea hospitali ya Wilaya ya Lulanzi, ya TANITA kuelekea chuo cha uongozi cha Mwl. Nyerere na Visiga -Zegereni na akawataka wakandarasi wanaotekeleza miradi hiyo kuzitendea haki fedha hizo nyingi zinazotolewa na Serikali kwa kutekeleza miradi kwa wakati bila ubabaishaji.
Kati ya fedha hizo, sh. Bilioni 21.111 ni kwa ajili ya mradi wa barabara inayojengwa kwa kiwango cha lami ya Visiga -Zegereni na Bilioni 1.367 kwa Ajili ya miradi ya dharura Kibiti, Mkuranga, Kibaha na Bagamoyo.
Mkuu huyo wa Mkoa alieleza kuwa TARURA na TANROADS Wana mahusiano mazuri ya kiutendaji wa kazi na kuwa wanafanya kazi kubwa.
Kunenge alifafanua kuwa TANROADS ilitengewa zaidi ya sh.bilioni 42 na Hadi Sasa wameshapelekewa asilimia 75 ya fedha hizo na TARURA imeshapelekewa asilimia 95 ya fedha zotewalizotengewa.
"Tunamshukuru Rais wetu, mkoa kautendea haki, kwa upande wa barabara hii ya Visiga -Zegereni Ni mradi unaokwenda Viwandani km 12.5 unatekelezwa na TARURA, Sasa utaona mradi huu unagharimu Bilioni 21 Hadi kukamilika Ni Jambo la faraja kwakuwa utasaidia wawekezaji kusafirisha malighafi na bidhaa zao kwa urahisi," alifafanua Kunenge.
Awali Meneja wa TARURA mkoa, Leopold Runji alisema wametengewa Bilioni 44.6 na kuwa tayari wameshapokea Bilioni 25.074 na kuwa mradi wa Visiga- Zegereni umefikia asilimia 10 ya utekelezaji hadi Sasa.
Runji alitaja mafungu ya fedha walizopokea kimkoa akisema “tumeshapokea kiasi cha sh. Bilioni 8.2 za mfuko wa barabara kwa ajili ya matengenezo ya barabara ya kawaida kilometa 873.98, za Mfuko wa Jimbo sh. Bilioni 4.8 na fedha za tozo sh. Bilioni 28.236.”
Naye Dereva bodaboda aliyejitambulisha kwa jina la Majid Muhammad alisema kwa sasa wanapata changamoto kipindi cha mvua hivyo wanaishukuru Serikali kwa mipango ya kuboresha barabara Hali itakayowawezesha kupita kwa urahisi.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.