Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhe. Abubakar Kunenge, amesema serikali ya mkoa imelenga kuifanya Pwani kuwa kinara wa ubunifu na utatuzi wa changamoto kwa njia za kimkakati, ili kuongeza tija katika utoaji huduma na kuvutia uwekezaji.
Mhe. Kunenge ametoa kauli hiyo leo Octoba 17 wakati wa kufunga mafunzo ya kujengea uwezo viongozi wakuu wa sehemu na vitengo wa Halmashauri ya Chalinze, yaliyofanyika katika Shule ya Uongozi ya Mwalimu Nyerere, Kibaha.
Amesema viongozi wanapaswa kutumia maarifa waliyojifunza ili kuleta matokeo chanya katika maeneo yao ya kazi, kwa kuibua fursa mpya na kuweka mazingira rafiki kwa wawekezaji.
“Tujitahidi kutumia mafunzo haya kutengeneza fursa na kuweka mazingira rafiki ya uwekezaji. Tunataka kuona matokeo chanya ya mlichojifunza hapa,” alisema Mhe. Kunenge.
“Mkoa wa Pwani unataka kuwa eneo la ubunifu na suluhisho endelevu kwa changa moto zinazoukabili.”
Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani, Pili Mnyema, amewataka wahitimu wa mafunzo hayo kuendeleza mawazo ya kimkakati yatakayowezesha utekelezaji wa miradi bunifu ya maendeleo, ili kupunguza utegemezi kwa Serikali Kuu.
Amesisitiza umuhimu wa viongozi kuendana na mabadiliko ya teknolojia na kutumia mbinu mpya za usimamizi ili kuongeza ufanisi na tija katika utoaji wa huduma.
Mafunzo hayo ya siku tano yamejikita katika kuimarisha uwezo wa viongozi kwenye masuala ya uongozi, ubunifu, utatuzi wa changamoto, na usimamizi wa rasilimali, yakiwa na lengo la kuboresha utoaji huduma kwa wananchi na kuchochea maendeleo endelevu katika Halmashauri ya Chalinze na Mkoa wa Pwani kwa ujumla.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.