MKuu wa mkoa wa Pwani, alhaj Abubakari Kunenge amewaasa wakuu wa wilaya mkoani humo kutokuwa chanzo cha kukwamisha jitihada za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan bali wakawatumikie na kuwahudumia wananchi.
Kunenge ameyasema hayo leo Januari 30, 2023 Mara baada ya kuwaapisha wakuu wa Wilaya za Rufiji na Mafia walioteuliwa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan Januari 25 Mwaka huu.
Walioapishwa leo na wilaya zao kwenye mabano ni Col. Samwel Kolombo (Kibiti) na Zephania Stephen Sumaye (Mafia).
Kunenge amewaasa wakuu hao wa wilaya kwenda kufanya kazi kwa karibu pamoja na kamati za amani ili kushughulikia na kusimamia kwa pamoja kupunguza masuala ya uhalifu akizitaja baadhi kuwa ni za mmomonyoko wa maadili kama vile ubakaji, na ulawiti na ambayo yanaonekana kushamiri.
Vilevile alieleza kuwa Mkoa wa Pwani ni wa biashara na uwekezaji hivyo wakuu hao wa wilaya wakaweke Mazingira bora ya uwekezaji kuvutia wawekezaji ili pia kuongeza vyanzo vya mapato.
"Twendeni tukawatumikie na kutatua kero zao wananchi, sisi ni watumishi wao, kwasababu CCM iliahidi kuwatumikia na wananchi wakaridhia, kuna mkataba wa wananchi na CCM kutekeleza ilani hivyo wajibu wetu ni kutekeleza ilani," alisema Kunenge.
Mkuu huyo wa MKOA pia alitoa msisitizo wa viongozi hao kushirikiana katika kuongeza mapato na kudhibiti upotevu wowote unaoweza kutokea akisema “Pamoja na hayo, mkafanye kazi na Halmashauri na Taasisi zote za Serikali kusimamia mapato ya halmashauri na kudhibiti utoroshaji wa fedha za mapato ambao wakati mwingine unafanywa na baadhi ya watumishi.”
Aisha, Kunenge aliwaasa wakuu wilaya kuhakikisha kuwa wanazijua wilaya zao kama viganja vyao vya mkono na kuzijua kero za wananchi wao na kuwatumikia na kuwa wawe wanatoka maofisini na kwenda kuzijua na kuzitatua kero za wananchi kwenye maeneo yao.
Awali, Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani, Zuwena Omari aliwasihi wakuu wa wilaya kijumla kwenda kusimamia mapato na mianya ya utoroshaji wa fedha za mapato ambao wakati mwingine unafanywa na baadhi ya watumishi.
Zuwena pia alizitaka Halmashauri kutumia mashine za kukusanyia mapato kwa njia ya kielektroniki ili kupunguza “upigaji” wa mapato.
Vilevile Katibu Tawala huyo alitoa rai kwa viongozi hao kusimamia asilimia 10 za mapato ya Halmashauri ambazo zinatengwa kwa ajili ya vikundi vya vijana, wanawake na makundi maalum.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.