Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhe. Mhandisi Evarist Ndikilo ameliagiza Jeshi la Polisi Mkoani Pwani, kuwasaka wale wote waliohusika kuwapa mimba wanafunzi 20 waliokosa kuhitimu elimu ya msingi mwaka huu.
Amesema, wanaume wanaowatongoza watoto wa kike waliopo shule, wanatakiwa kushtakiwa kwa mujibu wa sheria na kufungwa miaka 30 jela.
Akifungua kikao cha bodi cha matokeo ya wanafunzi kujiunga kidato cha kwanza mwaka 2018, Mhandisi Ndikilo alisema, Jeshi la Polisi lianze na wahusika hao kwakuwa wanajulikana.
Alieleza hataki kusikia mwalimu mkuu ama mzazi anakaa kumalizana na watuhumiwa wanaohusika kuwapa mimba watoto bali wahakikishe wanatoa ushirikiano ili wachukuliwe hatua stahiki. Aliwaasa wanafunzi wa kike kuacha kushawishiwa kwa chipsi, simu na badala yake wajikite kwenye elimu ambayo ni msingi wa maisha yao.
“Naagiza Jeshi la Polisi kuwakamata watu hao waliowatia mimba wanafunzi wakashindwa kufanya mitihani yao ya kumaliza darasa la saba mwaka huu,”
“Mifataki hii,inashindwa kuwafuata saizi zao wanaenda kuwarubuni watoto wa shule, wakashindane kwa hoja na wanawake walio saizi zao, sio kushindana kwa hoja ya chipsi,kuku,au simu” alisema Mhandisi Ndikilo.
Aliwapongeza walimu, Maafisa Elimu na waratibu wa Elimu Mkoani Pwani kwa kuongeza jitihada na kusababisha ufaulu kimkoa kwa mwaka huu kupanda na kufikia asilimia 66.9 na kusema kuwa ni hatua nzuri . Alibainisha, ufaulu umeongezeka katika halmashauri ikiwa ni sanjari na Kibiti 54.02 na Rufiji 52.94 licha ya Wilaya hizo kukumbwa na hali ya kiuhalifu kwenye kipindi hicho.
Katibu Tawala wa Mkoa Ndg. Zuberi Samataba ambaye alikuwa mwenyekiti wa kikao hicho alielezea, watahakikisha wahusika wanakamatwa na kufikishwa mahakamani. Aidha alisema kuwa, kila Halmashauri inawajibu kutafuta sababu zilizopelekea kufanya vibaya kwa shule hizo kumi ili kupata ufumbuzi wa haraka.
Samataba aliwataka walimu kutimiza wajibu wao na kuacha kutoroka nyakati za kazi na kwenda mijini kufanya mambo mengine “Walimu na wazazi washirikiane na Idara ya Elimu Wilaya na Mkoa kukabiliana na changamoto zinazosababisha taaluma kushuka ili kuhakikisha matokeo ya mwaka ujao yanapanda zaidi ya sasa” .
Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Elimu Ndg. Abdul Maulid alisema, wanafunzi 101 sawa na asilimia 0.37 hawakufanya mtihani kwasababu mbalimbali ikiwemo mimba. Wanafunzi wengine 60 ni watoro, vifo sita ,ugonjwa 12 na sababu nyingine.
Hata hivyo, Maulid alisema hali ya matokeo ya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi mwaka huu Mkoani Pwani, imepanda kutoka asilimia 62.57 mwaka 2016 hadi kufikia asilimia 66.9 mwaka 2017 sawa na ongezeko la asilimia 4.33.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.