Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhandisi Evarist Ndikilo amemtaka mmiliki wa Kampuni ya Mafubilo General Supplies kuwalipa wakulima wa korosho kiasi cha fedha shilingi milioni. 356,156,335.30
Fedha hizo ni deni wanalodai wakulima wa Kibaha baada ya korosho zao kilo 282,306.5 zilizokuwa kwenye vyama vya ushirika (AMCOS) vitano kuuzwa kwa Kampuni hiyo.
Ndikilo alitoa agizo hilo Machi 3, 2021 Mjini Kibaha wakati wa kikao maalum na wakulima ambao waliingiia mkataba na mfanyabiashara huyo.
Kutokana na deni hilo Mhandisi Ndikilo alitoa muda wiki moja kwa mfanyabiashara huyo kukiri kuwa atalipa deni hilo pindi tu atakapata barua ya kumtaka alipe.
Aidha amempa muda wa miezi mitatu kuhakikisha analipa deni hilo kwa awamu tatu (shilingi Milioni 118) akishindwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.
Kwa mujibu wa mkataba uliosainiwa mwezi Februari mwaka 2020 kati ya Kampuni ya Mafubilo na vyama hivyo vya ushirika ni kwamba mnunuzi alitakiwa kulipa fedha hizo kwa muda wa siku 63.
AMCOS zilizoingia mkataba huo ni Kongowe ( kilo 168,982.50), Mwendapole (kilo 2,279) na Misugusugu (kilo 72,314), Visiga (kilo 36,244) na Mkombozi ( kilo 2,487) na kwamba kilo zote za Korosho zina thamani ya Shilingi 394,156,335.30 hadi sasa ni Shilingi Milion 40 tu ambazo zimelipwa na Kampuni hiyo.
Wakulima hao wamemshukuru Mkuu kwa Mkoa kwa hatua hiyo nzuri na kusema kuwa wamekuwa wakisumbuka kwa muda mrefu kufatilia jambo hilo na kwamba sasa wameanza kuona muelekeo wa kupata haki zao.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.