Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhandisi Evarist Ndikilo ameshiriki na kushuhudia mnada wa kwanza wa Korosho kwa msimu wa mauzo wa 2019 Mkoani hapa ambapo jumla ya kilo 156,257 kwa Daraja la kwanza na la Pili zimeuzwa.
Katika mnada huo, Korosho Daraja la Kwanza ambazo ni kilo 46,781 zimeuzwa kwa bei ya shilingi 2,571 kwa kilo na kampuni iliyozinunua ni Alpher Choice Ltd. na Korosho daraja la Pili kilo 109,476 zimeuzwa kwa bei ya shilingi 2,300 na zimenunuliwa na kampuni CDJKL Nuts Ltd.
Akifungua mnada huo Mhandisi Ndikilo amewataka wanunuzi wote kuhakikisha kuwa wanalipa fedha hizo si zaidi ya siku kumi na kuichukua Korosho yao.
Katika hotuba yake ya ufunguzi wa mnada huo, Mhandisi Ndikilo amewataka wakulima wa Korosho Mkoani Pwani kuhakikisha wanatunza mikorosho yao kwa kuipalilia ili waweze kuzalisha Korosho zilizo na ubora mzuri na akaonya tabia ya baadhi ya watu kuweka mchanga na mawe kwenye magunia ya korosho kwani kufanya hivyo ni udanganyifu unaoliharibia zao hilo soko na unauletea Mkoa na Taifa sifa mbaya.
Awali Mhandisi Ndikilo alizungumza na wadau wa zao la Korosho kwenye kikao maalum kilichojadili mwenendo wa uzalishaji zao la Korosho changamoto za kuchelewa kufanyika mnada wa zao hilo kutokana na hali ya hewa kufuatia mvua nyingi kunyesha kwa Zaidi ya miezi mitatu.
“Baadhi ya AMCOS hazikuchambua na kupanga korosho katika madaraja kutokana na viwango vya ubora, hali iliyosababisha baadhi ya AMCOS kurudisha korosho kwa uchambuzi Zaidi na kufanya marekebisho yanayohitajika: alisema Mhandisi Ndikilo.
Mhandisi Ndikilo alifafanua kuwa hali hiyo ilisababisha uongozi wa Mkoa kukaa na viongozi wa chama kikuu cha CORECU na kufikia maamuzi kuwa AMCOS sasa zikusanye korosho kwenye maghala yao lakini wasisafirishe kwenda ghala kuu hadi uchambuzi uwe umefanyika.
Kwenye mkutano huo, Mhandisi Ndikilo amekemea tabia ya baadhi ya viongozi wa AMCOS kutumia Stakabadhi bandia kwa lengo la kuwadhulumu Wakulima na akaonya kuwa AMCOS zitakazobainika kuwaibia wakulima zitavunjwa zote na viongozi wao watachukuliwa hatua kali za kisheria.
Mhe. Ndikilo alisema kuwa hali ya mapokezi ya korosho kwenye maghala makuu bado sio nzuri.
Pia alisema kuwa zaidi ya kilo milioni 20 zinatarahiwa kukusanywa kutoka kwa wakulima kwa msimu wa mauzo ya mwaka huu wa 2019 na kwamba korosho nyingi zipo kwenye maghala ya AMCOS ambako zinaendelea kufanyiwa tathmini ya ubora na nyingine zimekaguluwa na kubainika kuwa na ubora hafifu ambao nje ya madaraja rasmi yanayotambuliwa na sheria ya Bodi ya korosho.
“Korosho zisizo na ubora ziendelee kuhifadhiwa hadi wadau watakapokaa na kuamua hatma ya Korosho hizo” aliongeza Mhandisi Ndikilo.
Kikao hicho kilifanyika Wilayani Mkuranga na kuhudhuriwa na wadau mbalimbali wa korosho wakiwemo Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi wa Halmashauri, wakulima wa zao la Korosha, wataalamu kutoka ofisi ya Mkuu wa Mkoa pamoja na wadau kutoka Bodi ya Korosho.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.