Mkuu wa mkoa wa Pwani Mhe.Mhandisi Evarist Ndikilo amewataka watu wote waliovamia maeneo yakiwemo ya shule yaliyotengwa kwa ajili ya michezo wayaachie maeneo hayo mara moja ili waweze kuwapisha vijana kutumia maeneo hayo kwa kuendeleza vipaji vyao vya michezo.
Aliyasema hayo mjini Kibaha wakati wa bonanza la michezo kimkoa la kumbukumbu ya maadhimisho ya miaka 58 Uhuru ambapo bonanza hilo lilifanyika katika uwanja wa Shirika la Elimu Kibaha Tumbi.
Mhandisi Ndikilo alisema kuwa ili kukuza vipaji vya michezo lazima kuwe na viwanja vingi vya michezo lakini baadhi ya watu wamekuwa wakiyavamia maeneo hayo na kusababisha vijana kukosa sehemu za kufanyia michezo.
"Wale wote waliovamia viwanja vya michezo kwenye Mkoa wangu waviachie ili vijana waweze kuendeleza vipaji sababu kama hakuna viwanja pamoja na vifaa vya michezo ni ndoto kwa Vijana wetu kuendeleza michezo", alisema Mhandisi Ndikilo.
Pia alisema kuwa Halmashauri za mkoa huo zihakikishe zinaendeleza vipaji vya wanamichezo na kuhakikisha kuwa watumishi wake wanashiriki michezo kwani ni sehemu ya kazi na kuboresha afya zao.
"Kuna changamoto ya fedha kwa ajili ya masuala ya michezo hivyo Serikali inalifanyia kazi suala hilo ili kuona uboreshaji wa michezo unafanikiwa," alionhezea Mhandisi Ndikilo.
Aidha alisema wawekezaji ndani ya mkoa watenge maeneo kwa ajili ya viwanja vya michezo ili wafanyakazi wapate muda wa kufanya michezo.
"Michezo ni ajira hivyo ni vema wadau mbalimbali wakajitokeza kuwekeza kwenye michezo ili kuunga mkono jitihada za serikali kwani vijana wanaweza kujiajiri kupitia michezo," alisema Ndikilo.
Kwa upande wake Afisa michezo mkoa wa Pwani Grace Bureta alisema kuwa wameamua kusherehekea sikukuu hii kwa kufanya michezo mbalimbali.
Bureta alisema kuwa mazoezi ni sehemu ya kazi na watumishi nao wanashiriki michezo hivyo ni sehemu ya burudani na kufurahia siku ya Uhuru wa nchi.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.