Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhe. Mhandisi Evarist, amewaagiza wakuu wa Wilaya zote za Mkoani hapa kuanza mara moja kuhamasisha wananchi kujiunga na mfuko wa afya ya jamii ulioboreshwa ili kusaidia serikali kufikia azma yake ya kutoa huduma za afya kwa wananchi wote kwa kutumia bima ya afya.
Mhandisi Ndikilo ametoa agizo hilo katika kata ya Miono iliyoko wilaya ya Bagamoyo wakati wa uzinduzi wa mfuko wa CHF iliyoboreshwa katika Mkoa huo mwanzoni mwa wiki hii.
Aidha mewataka wakuu hao wa Wilaya kushirikiana na viongozi wa kata kuhamasisha wananchi kuona umuhimu wa kujiunga na mfuko huo kwani umeboreshwa na kuongeza wigo ambao utamwezesha mwanachama kutibiwa katika hospitali zote ndani ya Mkoa huo tofauti na kipindi cha nyuma ambacho kilikuwa kinamlazimisha mwanachama kupata matibabu katika halmashauri anayotoka au alikojiandikishia.
Ametoa muda wa mwezi mmoja kwa halmashauri ambazo bado hazijaanza kutekeleza mpango wa uhamasishaji wananchi kuijiunga na CHF iliyoboreshwa kuanza zoezi hilo mara moja na kumfikishia taarifa ofisini kwake kabla ya tarehe 30 mwezi ujao ikionyesha namna ambavyo wamehamisisha wananchi kujiunga na mfuko huo.
“Napenda kutoa wito na kuziimiza halmashari ambazo hazijaanza utekelezaji wa CHF iliyoboreshwa kuhakikisha wanaanza mwezi huu wa juni 2019 na nipate taarifa rasmi ifikapo tarehe31 julai 2019 kwamba utekelezaji wa CHF iliyoboreshwa umeanza kazi kwenye halmashauri hizo” alisema Mhandisi Ndikilo
Akiongea kwa niaba ya wakuu wote wa wilaya za Mkoa huo , mkuu wa wilaya ya Mafia Shaibu Mnunduma amemhakikishia mkuu huyo wa Mkoa kuwa watasimamia kikamilifu mpango huo na kuhakikisha kila mwananchi anajiunga na mfuko huo.
Kwa upande wao baadhi ya wakazi wa kata ya Miono wameipongeza serikali kufanyia maboresho mfuko wa afya ya jamii kwa ili uweze kusaidia na kunufaisha wananchi wengi.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.