Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhe. Mhandisi Evarist W. Ndikilo amewasimamisha watumishi wawili wa kampuni ya ujenzi ya Yapi Merkezi ya nchini Uturuki inayojenga reli ya Standard Gauge kutoka Dar es Salaam - Morogoro kwa tuhuma za rushwa ya ajira.
Aidha ameagiza watumishi hao wasimamishwe kupisha uchunguzi huku akitoa siku saba kwa vyombo vya dola kufuatilia suala hilo.
Mhe. Ndikilo, aliyasema hayo wakati alipotembelea ujenzi wa mradi huo kwenye kijiji cha Soga wilayani Kibaha.
alieleza kuwa endapo ikibainika wamehusika na vitendo hivyo hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.
Aliwataja watumishi hao ambao walikuwa wakilalamikiwa na wananchi waliokuwa wakienda kuomba kazi kuwa walikuwa wakiomba rushwa ni pamoja na Nelson ambae ametambulika kwa jina moja Afisa mwajiri(HRO) kwenye kampuni hiyo.
Mwingine ni Torong’ong’o ambaye ni dereva wa moja ya viongozi wa kampuni hiyo ambao hawakuhudhuria hata kwenye mkutano huo.
Awali Mhandisi Ndikilo alipokelewa kwa mabango na watu waliokuwa nje ya kampuni hiyo wakilalamika kunyimwa ajira za udereva na uendeshaji wa mitambo wakidai kuwa ajira zinatolewa kwa njia ya rushwa.
“Tunanyimwa ajira hasa tunaotoka maeneo ya Kibaha na Mkoa wa Pwani kwa ujumla na wanaoajiriwa ni watu wa nje ya Mkoa” walisema.
Mhandisi Ndikilo, alielezea kwamba alikuwa pia akipelekewa malalamiko ofisini kwake ambapo baadhi ya madereva waliandika majina yao na kuambatanisha vyeti vyao na uzoefu wao wa kazi lakini hawakupata ajira.
“Malalamiko yamekuwa ni mengi sana na wanaolalamika wanasema wamenyimwa ajira wengi ni wa hapa Kibaha na Mkoa wa Pwani ambao walipaswa kunufaika na mradi huu kwani kila eneo lenye mradi lazima wahusika wa eneo wapewe kipaumbele, inadaiwa walioajiriwa, wenyeji hata 100 hawafiki katia ya 390 ya walioajiriwa,” alisema Ndikilo.p
Kwa upande wake Meneja wa mradi huo ulio chini ya Reli Assets Holding Company (RAHCO), Mhandisi Maizo Mgedzi alisema kuwa watahakikisha wanalifuatilia suala hilo ili kupisha uchunguzi lengo likiwa ni kuhakikisha hakuna malalamiko kwa wananchi wanaozunguka eneo la mradi huo.
Naye mwakilishi wa kampuni ya Yapi Merkezi Mhandisi Mert Oz alisema, endapo watabaini wapo walioingizwa kwenye ajira kinyume cha utaratibu, hawatasita kuwaondoa.
Mhandisi Oz alisema, wanafuata taratibu za ajira na wanategemea kuletewa wafanyakazi kwa utaratibu wa nchi na kufuata sheria za ajira.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.