MKuu wa Mkoa wa Pwani Mhandisi Evarist Ndikilo ametoa rai kwa viongozi wa dini kuwashirikisha waumini wao kwenye nyumba za ibada kuliombea Taifa kuelekea siku ya kupiga kura tarehe 28 mwezi huu ili ufanyike kwa utulivu na amani.
Mhe. Ndikilo ametoa rai hiyo leo Oktoba 26, 2020 katika kikao cha kamati ya amani ya Mkoa kilichofanyika kwenye ukumbi wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani-Kibaha.
Alisema, Mkoa umekamilisha maandalizi yote kwa ajili ya kupiga kura siku hiyo ya Octoba 28 na kwamba yote hayo hayawezi kufanyika bila huruma ya Mungu.
Mkuu huyo wa Mkoa alisema, ni jukumu la viongozi wa dini kuzidisha maombi kuomba amani ili kura zipigwe kwa amani na utulivu na mshindi atangazwe bila shinikizo.
Alisema, Serikali inahakikisha uchaguzi unafanyika kwa amani na utulivu, na kwamba Mkoa unatarajia baada ya kupiga kura, zihesabiwe kwa utulivu na mshindi kutangazwa bila kikwazo ili mkoa uendelee kubaki na hali ya amani baada ya Uchaguzi.
Aliwasisitiza wananchi wenye sifa kujitokeza kupiga kura ili kutimiza wajibu wao na kuzingatia kikamilifu maelekezo kutoka tume ya Uchaguzi.
Nae Mwenyekiti Mwenza wa kamati ya amani ya Mkoa wa Pwani Hamis Mtupa alisema kipindi chote cha Kampeni hapakuwa na uvunjifu wa amani hivyo kuwaomba wananchi kuendeleza hali hiyo ya utulivu siku ya Uchaguzi.
Alisisitiza wananchi kurudi nyumbani baada ya kupiga kura, huku akitoa tahadhari kwa Jeshi la polisi kuhusiana na mkesha wa maulidi ambao utakuwa siku ya kupiga kura.
Kwa upande wake Padri Benno Kikudo alisema wanaendelea na maombi kuiombea nchi kufanya uchaguzi kwa amani huku akiwasihi wagombea kuwa tayari kupokea matokeo baada ya kura kupigwa.
Akichangia wazo, Ahmad Seif mmoja wa wajumbe wa kamati ya amani aliiomba Serikali kuwezesha kamati hiyo ya mkoa kufika maeneo ya shule kuwaelimisha Vijana umuhimu wa kulinda amani.
Seif alisema Serikali inatakiwa kuangalia namna ya kutengeneza amani kuanzia shuleni kwani kundi la Vijana ndio linalochangia kupotea kwa amani.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.