Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhandisi Evarist Ndikilo amewataka wakuu wa Wilaya za Mkoa huo ambao hawajatekeleza agizo la kutengeneza madawati kumpa malelezo ya sababu zilizowakwamisha.
Akiongea wakati alikabidhiwa madawati na Mkuu wa Wilaya ya Rufiji Luteni Kanali Patrick Sawala mjini Kibaha, Ndikilo alisema agizo hilo alilitoa mwezi mmoja uliopita lengo likiwa ni kumaliza tatizo la watoto kukaa chini katika Mkoa huo.
"Wakuu wa Wilaya ambao hawajakamilisha kutengeneza madawati nipate maelezo ya kina yenye sababu za mashiko tujue kwanini hawajakamilisha hadi sasa" alisema Ndikilo.
Mkuu huyo alisema, Mkoa huo umejipanga kuhakikisha hakuna mwanafunzi anayekaa chini, ili wanafunzi wapate Elimu katika Mazingira bora.
" Tulikubaliana na Wakuu wa Wilaya katika kikao kazi tulichoketi mwezi mmoja uliopita hatuwezi kuwa na watoto wanaokaa chini na tarehe moja leo ndio ilikuwa mwisho" alisema.
Alisema kuwa , uwepo wa madawati ya kutosha shuleni itamsaidia mwanafunzi kuacha utoro, na mwalimu atakuwa anafundisha katika Mazingira mazuri .
Aidha Ndikilo aliwahimiza wakurugenzi kuacha kukimbilia kutengeneza madawati, Viti na meza kwa beii rahisi na badala yake kwenda sehemu ambazo zinamatengenezo yenye ubora .
" Madawati haya yanayotengenezwa hapa katika shirika la Nyumbu ni tofauti na mitaani, yanauwezo wa kudumu kwa miaka mitano tofauti na huko mtakakoenda ambako kila mwaka mtakuwa mnatenga bajeti kukarabati au kutengeneza upya" alisema Ndikilo
Nae Katibu Tawala Mkoa wa Pwani Dkt Delphine Magere alimpongeza Mkuu wa Wilaya ya Rufiji kwa kutekeleza agizo la Mkuu wa Mkoa kwa wakati.
Alisema Kauli mbiu ya Pwani hakuna kukaa chini itatekelezwa kwa vitendo kwani Mkoa huo ni wapiganaji wanaopigania nchi na kwahivyo nchi itakuwa na wasomi wakupeleka uchumi mbele.
Akimkabidhi madawati hayo kwa Mkuu wa Mkoa , Mkuu wa Wilaya ya Rufiji Luteni Kanali Patrick Sawala alisema, Wilaya hiyo ilikua na mapungufu ya meza 1882, Viti 231 na madawati 3945 na kwamba wamejipanga kuhakikisha wanatekeleza mpango huo.
Alimshukuru Mkurugenzi wa Shirika TACT Nyumbu kwa kumaliza matengenezo ya Viti na meza 300 kwa wakati.
Mkurugenzi wa Shirika TACT Nyumbu Brigedia General Hashimu Komba alisema, mwitikio ni mkubwa kwa watendaji kuitikia agizo la Mkuu wa mkoa kutumia Shirika hilo kutengeneza madawati, Viti na meza zinazohitajika.
Alisema, mbali ya kukamilisha viti na meza kwa ajili ya Rufiji pia wanatarajia kukabidhi viti na meza 400 kwa ajili ya Wilaya ya Mkuranga.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.