MKuu wa Mkoa wa Pwani, Mhe. Mhandisi Evarist Ndikilo amewataka wakazi wanaoishi maeneo ya mabondeni ambayo yana athari kubwa kwa mvua ,huko Muhoro na Chumbi ,Wilayani Rufiji kuhamia maeneo ya yaliyo salama kwako ili kujiepusha na maafa na madhara makubwa kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha.
Amesema ,hadi sasa maafa tayari ni makubwa na takwimu zilizofika mkoani hadi sasa ni takriban hekta 6,600 za mashamba na makazi ya watu zimeathirika ,kituo cha afya kimezingirwa na maji hakitoi huduma pamoja na kaya 3,500 zimekumbwa na maafa hayo.
Ndikilo alitoa kauli hiyo, baada ya Mwenyekiti wa kijiji cha Muhoro Magharibi, Amin Mnyimwa wakati akitoa kilio chao kuhusu mafuriko yalivyowaathiri na kukubali wahamishwe maeneo mengine ili kunusuru maisha yao.
Mhandisi Ndikilo alieleza, kutokana na athari hiyo kamati ya usalama Mkoa na Chama Cha Mapinduzi (CCM)kimelazimika kwenda kujionea hali halisi ya majumba ,mazao mbalimbali kuzama katika maji.
Aidha alisema kuwa serikali inafanya juhudi za kuwahamisha na kukamilisha taratibu ya kuzungumza na wakala wa misitu (TFS) ambayo ipo chini ya Wizara ya maliasili na utalii.
Pia alifafanua kuwa,wataangalia namna ya kuhamisha shule na kituo cha afya .
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Rufiji,Juma Njwayo alithibitisha kuwa, eneo hilo halifai kabisa kuishi kabisa kutokana tatizo la mafuriko ya mara kwa mara.
Nae mwenyekiti wa kijiji cha Muhoro, Muharami Mkumba alibainisha, kijiji hicho kina vitongoji vinne kati yake vitatu vimekumbwa na adha ya maji na kaya 580.
Katika hatua Nyingine Mhandisi Ndikilo ametoa wito kwa wakazi wa Rufiji kuendelea kuchukua tahadhari kwani wataendelea kupata maji mengi kutokana na kufunguliwa kwa mabwawa ya Mtera na Kidatu na Mvua zinaendelea kunyesha Nyanda za juu Kusini.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.