MKuu wa Mkoa wa Pwani Mhe. Mhandisi Evarist Ndikilo ambae ni Mwenyekiti wa Kamati ya Usalama Mkoa l Desemba 14, 2020 amefungua Kikao kazi cha Mwaka cha Watendaji wa Jeshi la Akiba Mkoa wa Pwani.
Akizungumza kwenye Mkutano huo Ndikilo ameelekeza Wakurugenzi wa Halmashauri zote za Mkoa wa Pwani kushirikiana na Ofisi za Washauri wa Jeshi hilo katika kutumia Vijana wanaohitimu mafunzo ya Mgambo kutekeleza majukumu ya ulinzi na shughuli za Maendeleo ikiwemo ukusanyaji mapato kwenye Wilaya zao.
"Suala la Ulinzi na usalama ni jukumu la Mkurugenzi wa Halmashauri, hawa vijana waliohitimu mafunzo ni Wazalendo na wamefundishwa vizuri wanaweza kushiriki kwenye masuala ya Ulinzi na Shughuli za Maendeleo ikiwemo ukusanyaji mapato kwenye vitongoji, Kata na Tarafa zetu" alisema Ndikilo.
"Vijana hawa watengenezewe utaratibu mzuri wa kushiriki kwenye Ulinzi na usalama na Shughuli zingine za maendeleo kwenye Mkoa wetu kwa kufanya hivyo kutawapatia ajira na kuzuia uhalifu" alisisitiza Ndikilo. Aidha, amemtaka Kamanda wa Polisi na Vyombo vya Ulinzi Mkoani hapo kuendelea kuchunguza na kuzifuatilia kampuni za Ulinzi Mkoani hapo kama zinaajiri watu wenye sifa na waliopitia mafunzo ya Mgambo
Kuhusu Uandikishaji wa Vijana wa Jeshi la Kujenga Taifa Ndikilo amewataka watendaji wa Jeshi la Akiba Mkoani hapo kutenda haki na kuchagua vijana wenye sifa na vigezo wakati wa michakato hiyo kila Mwaka. " tumieni kikao hichi kutathimini michakato ya uandikishaji iliyoisha mapema mwezi huu na kujisahihisha pale ambapo kulikuwa na mapungufu" Ni aibu kubwa Kama kutakuwa Vijana mliowachukua wakawa sio raia watanzania, wagonjwa, wajawazito,na kukosa sifa ambazo zilihitajika Ni mambo ambayo yataleta doa kwenye Mkoa wetu alisema Ndikilo.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.