.
Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhandisi Evarist Ndikilo ametoa rai kwa wamiliki wa Viwanda ndani ya Mkoa huo kuzingatia haki na maslahi ya wafanyakazi wao.
Ndikilo alitoa rai hiyo wakati alipotembelea Kiwanda cha kuunganisha magari kilichopo eneo la Tamco Halmashauri ya mji wa Kibaha.
Alisema, ajira zinazotolewa kwa wafanyakazi zinatakiwa kuendana na haki ikiwemo vitendea kazi pamoja na maslahi na Afya zao wakiwa kazini.
"Baadhi ya wamiliki hawazingatii haki na maslahi ya wafanyakazi wao, wanawajali pale wanapokuwa wazima na kufanya kazi kwa bidii wakipata matatizo hawana habari nao, niwaombe kuheshimu wafanyakazi na kuwajali muda wote wakiwa kazini na wanazokumbana na matatizo" alisema Ndikilo
Aidha mkuu huyo wa Mkoa aliwataka wamiliki hao wa Viwanda kutumia benki zilizopo ndani ya mkoa huo, kupitisha fedha zao na kuomba mikopo lengo kukuza pato la Mkoa huo na Taifa kwa ujumla.
Alitoa wito kwa Taasisi wezeshi za Mkoa huo kujipanga vizuri kutoa vibali kwa wawekezaji ili shughuli za Uwekezaji zifanyike kwa wakati.
Awali meneja wa Kiwanda hicho Ezra Mereng alisema Kiwanda hicho Cha kuunganishiwa magari kitakapokamilika kitakuwa na Uwekezaji wa zaidi ya bilioni 12.
Aliongeza kuwa malengo yao ya baadae ni kuwa na ajira 300 za moja kwa moja na zisizorasmi 700 ambapo kwasasa zipo ajira 65 pekee.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.