Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhe. Mhandisi Evarist Ndikilo amezipongeza Halmashauri zote za Mkoa huo kwa kupata hati safi kwa mwaka 2017/2018.
Akifungua mafunzo ya siku moja ya kuzijengea uwezo Kamati za Ukaguzi za Halmashauri za Mkoa wa Pwani Mhandisi Ndikilo alisema taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali - CAG inaonesha kuwa halmashauri zote tisa za mkoa huo zimepata hati safi na akazipongeza kwa hatua hiyo.
Hata hivyo, mhandisi Ndikilo alisisitiza kuwepo usimamizi thibiti katika halmashauri ili kuhakikisha hoja za ukaguzi ambazo zimekuwa zikijirudia zifungwe kwa kukamilisha mapungufu yaliyopo.
Mhe. Mhandisi Ndikilo amezitaja baadhi ya hoja hizo kuwa ni ukosefu wa hati za malipo wakati wa Ukaguzi huku nyaraka hizo zikitolewa maelezo kuwa zilichukuliwa na taasisi zingine kama vile Taasisi ya kupambana na kudhibiti Rushwa - TAKUKURU pamoja na Polisi kwa hatua za utekelezaji wa majukumu yao.
“kwa kuwa taasisi hizo zipo Mkoani hapa, ni wazi kuwa nakala ya nyaraka hizo zinaweza kupatikana au zikaletwa akazifanyia kazi Mkaguzi kisha zikarudishwa tena kwenye taasisi hizo kuendelea na uchunguzi wao” alishauri mhandisi Ndikilo.
Akizungumzia umuhimu wa Mafunzo ya kuzijengea uwezo Kamati za Ukaguzi za Halmashauri, mkuu huyo wa Mkoa wa Pwani aliwaeleza washiriki kuwa watumie fursa hiyo kujadili namna watakavyoweza kuondokana na hoja za miaka ya nyuma ambazo hazijafungwa pamoja na changamoto nyingine zinazowakabili katika utendaji wao wa kazi ili Mkoa uendelee kupata hati safi.
“Ni matumaini yangu kuwa mada mbalimbali zitakazotolewa zitakumbusha wajibu wa utekelezaji wa majukumu yenu kama wajumbe wa kamati za ukaguzi na vipi kamati hizi zina mchango mkubwa kwa kila mshiriki katika kufanikisha malengo ya Halmashauri” alifafanua Mhandisi Ndikilo.
Aidha alisema kuwa mafunzo hayo yameandaliwa kama moja ya mikakati ya mkoa na Taifa ya kupambana na changamoto mbalimbali zinazojitokeza katika utekelezaji na usimamizi wa miradi ya maendeleo kwa Halmashauri na akaongeza kuwa lengo kuu la kuundwa kamati za ukaguzi katika Halmashauri ni kumsaidia Mkuregenzi kuzuia hoja zisitokee na kupendekeza namna bora ya kuwepo udhibiti wa ndani.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.