MKuu wa Mkoa wa Pwani, Mhandisi Evarist Ndikilo ametoa siku tatu kwa Jeshi la Polisi Chalinze, kuhakikisha wanawakamata wafugaji wawili wanaoishi Msata, Julius Nyangura na Denis Kichele kwa kosa la kudaiwa kutishia kuua na kulisha mifugo yao katika bustani ya mzee Seleman Salum.
Aidha ametoa mwezi mmoja wa majaribio kwa watendaji wa kata,vitongoji na vijiji Msata, wenyeviti wa vijiji wajitathmini na kusema akisikia mgogoro wa wakulima na wafugaji tena hatosita kuvunja serikali ya kijiji.
Ndikilo alitoa maagizo hayo ,wakati wa ziara yake ya kusikiliza kero za wananchi Msata ,huko Chalinze ambapo aliambiwa baadhi ya wafugaji katika eneo hilo wananyanyasa wakulima na kutamba kuiweka serikali ya kijiji mfukoni.
Alieleza wafugaji hao wahakikishe wanalipa pia fidia ya sh.milioni moja baada ya kulisha mifugo yao kwenye bustani hiyo ya robo heka iliyolimwa nyanya na mbogamboga mbalimbali.
Alisema endapo kama agizo hilo halitatekelezwa atawasiliana na IGP kumweleza tabia ya baadhi ya polisi kuwapa nguvu wafugaji ambao ni wakosaji.
"Haiwezekani polisi imuombe mkulima awasamehe wafugaji kutolipa fidia wakati wenzao wamepata hasara,jeshi lipo kwa ajili ya kutenda haki na kulinda amani ,hii itakuwa dawa, na lazima kuanzia sasa mtende haki bila upendeleo."
Ndikilo alifafanua, hawezi kulea watendaji wasio simamia majukumu yao ya kazi na kuendekeza kulea wahalifu ,na wakishindwa kuwajibika kuanzia sasa watachukuliwa hatua za kinidhamu.
" Hawa wafugaji wanawapa nini, kwanini mnawakingia kifua ,acheni kuwalinda ili kuondoa migogoro hii ya kila kukicha baina ya wakulima na wafugaji Chalinze,Bagamoyo na mkoa kijumla."alisisitiza Ndikilo.
Mkuu huyo wa mkoa alisema ,waziri mkuu na Rais wanapiga kelele kila kukicha kutoa rai kwa wafugaji kuheshimu wakulima na wakulima kuheshimu wafugaji ili kulinda amani.
Akizungumzia bonde la mto Ruvu alibainisha ,kila mmoja ana haki ya kulitumia pasipo kuvunja sheria ,na wale waliodaiwa fidia kulisha mifugo kwenye mazao ya wakulima milioni 50 ameshatoa agizo walipe.
Awali mzee Seleman alisema kwamba, July 10-16 July ndio chanzo cha mgogoro huo, wafugaji hao waliingiza mifugo yao katika bustani yake na kisha alitoa taarifa kwa mwenyekiti wa kitongoji Zunga na Msata na polisi .
" Polisi baada ya siku mbili waliniita na kuomba niwasamehe na siku iliyofuata alishangaaa kutishiwa kuuawa na wafugaji hao na kuambiwa kachinja ng'ombe watatu shambani kwake na mmoja kapotea ,jambo ambalo kwa uzee wake ni ngumu kulifanya."
Anadai mwisho wa siku alikubali kusamehe ili kuokoa uhai wake na baada ya kusikia kuna ziara ya mkuu wa mkoa alishukuru na kutoa dukuduku lake hilo.
Nae mkuu wa wilaya ya Bagamoyo, Zainab Kawawa alisisitiza upendo na kuishi kwa kuheshimiana kati ya makundi hayo ili kupunguza migogoro isiyo na tija.
Akizungumzia mgogoro baina ya kijiji cha Pongwe Msungura na jeshi Msata alisema kamati ya usalama ilifuatilia,ambapo 2005 serikali ilitwaa eneo hilo licha ya kwamba bado wahusika hawajalipwa fidia zao.
"Tulipata malalamiko wananchi wanadai kupigwa na kuchomewa vibanda vyao vya biashara, tulizungumza na kambi husika na kuagiza uongozi kuishi bila migongano na kuomba ramani iwasilishwe ili ijulikane mipaka halisi kati yao"alisema Zainab.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.