Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhe. Abubakari Kunenge, ameielekeza Mamlaka ya Mapato Tanzania -TRA- mkoani humo kuandaa utaratibu mzuri utakaowavutia wafanyabiashara kuendelea kulipa kodi kwa hiari, ili kuiwezesha serikali kupata fedha za kuendesha miradi ya maendeleo.
Kunenge ametoa wito huo leo Septemba 24, 2025 wakati wa uzinduzi wa dawati maalum la uwezeshaji biashara kwa mkoa wa Pwani ulifanyika katika ofisi za TRA zilizopo kibaha Mkoani Pwani.
Aidha, amesisitiza kuwa serikali inalenga kuhakikisha mkoa huo unakusanya mapato ya kutosha na kuwa kinara wa ukusanyaji wa kodi kutokana na wingi wa vyanzo vya mapato vilivyopo.
Amesema kuwa ni dhamira ya serikali kuona kuwa kila mwananchi anayestahili kulipa kodi anatimiza wajibu huo kwa hiari, bila kushurutishwa, na hivyo kuchangia kwa namna moja katika maendeleo ya taifa.
Kwa upande wake, Meneja wa TRA mkoa wa Pwani, Masawa Masatu, amesema lengo la kuanzishwa kwa dawati hilo maalum ni kuwa na chombo cha pamoja kitakachotumika kutatua changamoto mbalimbali za kikodi kwa wafanyabiashara kwa wakati muafaka.
Uzinduzi wa dawati hilo ni sehemu ya jitihada za serikali katika kuboresha mazingira ya biashara na kuhakikisha ukuaji wa uchumi katika mkoa wa Pwani.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.