Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhandisi Evarist Ndikilo amesitisha likizo kwa wakuu wa Wilaya na wakurugenzi wa Halmashauri za Mkoa huo hadi pale watoto waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza watakapokuwa wameaza masomo Januari 11 mwaka 2020.
Ndikilo alitoa agizo hilo wakati akiweka jiwe la msingi katika shule ya msingi Chatembo iliyopo kata ya Mwandege Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga.
Alisema viongozi hao wanatakiwa kuhakikisha miundombinu ya madarasa na madawati vinakamilika na kuwawezesha wanafunzi waliofaulu kujiunga na kidato cha kwanza wanapata nafasi wote.
Kwa mujibu wa Mkuu wa Mkoa wanafunzi waliofaulu 30197 ambao wanatakiwa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka 2021, na kwa Wilaya ya Mkuranga ni 7360.
"Maelekezo yangu haya yatawahusu pia walezi wa Wilaya nao hawatakuwa na likizo tujitahidi watoto waliofaulu wote wapate nafasi ili waliofaulu waone ni neema sio adhabu" alisema
Katika hatua nyingine Ndikilo amemuagiza meneja wa Tanesco kuhakikisha shule hiyo ya Chatembo inaunganishiwa nishati ya umeme mapema shule itakapofunguliwa mwezi Januari umeme uwe unawaka
Alimtaka meneja wa wakala wa barabara za Vijijini na mjini (TARURA) kusimamia ukarabati wa barabara inayofika katika shule hiyo kuondoa kero ya uwepo wa madimbwi yanayohifadhi maji katikati ya barabara.
"Ikifika Januari nipate taarifa ya ukarabati wa barabara hii nimeishuhudia ubovu uliopo na nitakapoitisha kikao cha bodi ya barabara nipate majibu kama utakuwa bado hujatekeleza usifike kwenye hicho kikao" alisisitiza
Awali Afisa Elimu msingi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga Jesi Mpangala alisema ujenzi wa shule ya msingi Chatembo ulianza mwezi Septemba mwaka huu na kwasasa umefikia hatua za umaliziaji.
Alisema kiasi Cha Shilingi Milion 400 kutoka Serikali kuu kilitolewa kwa ajili ya shule hiyo na vyumba 14 vya madarasa, jengo la utawala, matundu ya vyoo vya wanafunzi na walimu pamoja na nyumba za walimu vipo hatua ya umaliziaji.
Jesi alisema ifikapo Januari zaidi ya wanafunzi 2000 watahamia katika shule hiyo kutoka shule ya msingi Mwandege na kipaumbele kitakuwa kwa wale wanaoishi maeneo ya karibu na shule hiyo.
Aliishukuru Wizara ya maliasili kwa kukubali kutoa eneo hilo la ekari 15 kwa ajiili ya ujenzi wa shule hiyo.
Mbunge wa Jimbo la Mkuranga Abdallah Ulega aliishukuru Serikali kwa kutoa fedha hizo zilizojenga shule hiyo na kupunguza mlundikano katika shule ya msingi Mwandege inayoelezwa kuwa na wanafunzi 4,215.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.