Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge, leo amezindua mafunzo ya kozi ya uongozi na Menejiment bora kwa Wakuu wa Vitengo kutoka mashirika ya za umma.
Mafunzo haya yanafanyika leo Oktoba 21,2024, katika Shule ya Uongozi ya Mwalimu Julius Nyerere iliyopo Kibaha, mkoani Pwani.
Kunenge amewataka washiriki, baada ya kumaliza mafunzo hayo, kufanya kazi kwa kuzingatia vipaumbele vya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambavyo ni Maridhiano, Ustahimilivu, Mageuzi, na Kujenga Upya Taifa.
Kunenge alieleza kuwa kufahamu vipaumbele katika utendaji kazi kutasaidia kufikia malengo ya kuongeza tija, kuboresha utoaji wa huduma bora kwa wananchi, na kuhakikisha viwango vya kimataifa vinazingatiwa, ambavyo ndiyo dira ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
“Nyinyi ni viongozi mnaosimamia menejimenti, ambao mnachukua maamuzi muhimu. Mna nafasi kubwa ya kuunda mazingira bora kwa wafanyakazi wengine kufanya kazi vizuri, na kuhakikisha mifumo ya taasisi inaboreshwa.
Aliendelea kusema kuwa, Matarajio ya Rais ni kuona taasisi za umma zinatoa huduma bora kwa wananchi na wawekezaji ili kuboresha mazingira ya uwekezaji, kuongeza tija, na kutoa huduma za viwango vya kimataifa. Hii ndiyo kazi yenu,” alisema Kunenge.
Aidha, aliwakumbusha washiriki kuwa ni vigumu kutekeleza mambo mengi kwa wakati mmoja kutokana na rasilimali zilizopo, hivyo ni muhimu kuweka vipaumbele vya msingi vinavyoweza kuongeza tija kwa wananchi. Pia alisisitiza umuhimu wa kushirikiana, kuweka malengo yanayopimika, na kufanya tathmini ya utendaji kulingana na mahitaji ya wananchi, ambao ndiyo wateja wao wakuu.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.