Mkoa wa Pwani umeweza kupata vikombe Vikombe vitano na jumla ya Medali 34 katika mashindano ya UMISSETA na UMITASHUMTA kitaifa.
Akikabidhi vikombe hivyo kwa katibu Tawala Mkoa wa Pwani, Afisa Elimu mkoa huo Sara Mlaki amesema Mkoa wa pwani uliweza kushiriki mashindano hayo na kupata Vikombe 5 na medali 29 katika mashindano ya UMISSETA na Medali 5 katika mashindano ya UMITASHUMTA.
Akifafanua zaidi alieleza kuwa vikombe hivyo vitano ambavyo Mkoa ulivipata vilikuwa vya Mshindi wa kwanza Riadha Wanawake, Mshindi wa tatu riadha wanaume, Mshindi wa Pili mpira wa Mikono (Handball), Mshindi wa pili Ngoma na mshindi wa Pili Muziki wa Kizazi kipya.
Mlaki amesema mbali na makombe hayo matano, pia mkoa umepata vyeti viwili vya mshindi wa pili kitaifa ngoma na mshindi wa pili kitaifa Muziki wa kizazi kipya.
Sara alifafanua kuwa kwa upande wa medali 29, kati ya hizo 21 ni za Dhabhabu, 6 za Fedha na 2 ni za Shaba.
"Pamoja na changamoto nyingi zilizokuwa zikitukabili lakini tukiwa kama timu ya mkoa tuliweza kushikamana kwa pamoja, tukapambana na kuleta mafanikio haya ambapo katika mashindano ya UMISSETA tuliweza kushika nafasi ya 14 na UMITASHUMTA nafasi ya 18 kitaifa," alisema Mlaki.
Akipokea Vikombe hivyo Katibu Tawala Mkoa wa Pwani ambaye pia ni Skauti Mkuu wa Tanzania Rashid Mchatta amezipongeza timu hizo za UMISSETA na UMITASHUMTA kwa kujitahidi kufanya vizuri na kuwataka waongeze juhudi zaidi ili kuweza kuleta vikombe vyote vya mshindi wa kwanza.
"Kwa kweli nawapongeza sana kwa hatua mliofikia na kujitahidi hadi kuleta vikombe hivi vitano na na Medali hizi 34, pamoja na changamoto zote lakini mmeweza kufanya vizuri hivyo kwa mwaka ujao naamini hizi changamoto hazitajitokeza tena na hivyo mtafanya vizuri zaidi," alisema Mchatta.
Mashindano ya UMISSETA na UMITASHUMTA mwaka huu kitaifa yalifanyika mkoani Tabora na yalijumuisha mikoa yote Tanzania.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.