Serikali imetenga eneo la ukubwa wa hekta 60,000 kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji wa zao la mpunga katika wilaya ya Rufiji mkoani Pwani.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa kauli hiyo leo Septemba 20, 2023, wakati akiwasalimia wananchi wa Kata ya Ikwiriri wilaya ya Rufiji mkoani Pwani.
Amesema kwa mwaka huu wamekusudia kulima hekta 30,000 za mpunga kupitia skimu ya umwagiliaji ambayo serikali imetenga kwa ajili ya shughuli za kilimo na kwamba mwaka ujao watalima hekta zingine 30, 000.
“Tumeamua kugawa eneo la bonde la Rufiji kwa ajili ya shughuli za kuzalisha umeme na nusu yake skimu za umwagiliaji na mwaka huu tunaanza kulima hekta 30,000, zitazokuwa mahsususi kwa ajili ya kulima mpunga ambao utalisha mataifa mbalimbali kutokea hapa Rufiji," mesema Rais Dkt. Samia.
Kwa hali hiyo, amewahamasisha vijana kuchangamkia fursa hiyo ya kilimo cha umwagiliaji kupitia mradi wa Jenga Kesho iliyobora (BBT) kwa kuzalisha mpunga kwa wingi ambao utauzwa ndani na nje ya nchi kutokana na kuwepo kwa soko la uhakika.
Kwa upande wake, Mkuu wa mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge, amemshukuru Rais Dkt. Samia kwa kutoa bure pembejeo za kilimo ikiwamo mbolea ya ruzuku katika zao la korosho ambalo ameeleza kuwa kutokana na hatua hiyo ubora na uzalishaji wa zao hilo umeongezeka.
Amesema kwa sasa wanapata bure pembejeo aina ya sulphur ambayo hapo awali walikuwa wanapata changamoto ya kumudu gharama za kununa pembejeo za kilimo.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.