Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa ameeleza kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan ataendelea kutoa fedha za miradi mbalimbali ya Maendeleo huku akiagiza miradi yote kutekelezwa kulingana na thamani ya fedha hizo na kuwa kinyume na hapo wahusika watachukuliwa hatua kali za kisheria.
Mhe. Majaliwa alieleza hayo wakati akitoa ufafanuzi kufuatia maombi mbalimbali yaliyowasilishwa kwake na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Mkuranga Mhe. Abdallah Ulega aliyewasilisha maombi mbalimbali ikiwa ni pamoja na la ujenzi wa hospitali mpya ya Wilaya, ujenzi wa kituo cha magari ya abiria (stendi ya mabasi) Kipala mpakani na Ujenzi wa barabara ya Mkuranga hadi Kisiju ambako kuna bandari ya kihistoria.
Kuhusu ombi la ujenzi wa barabara ya Kisiju, Mhe. Majaliwa aliiagiza TANROAD kufanya utaratibu wa kuiweka kwenye mpango na alifafanua kuwa kuna mpango wa kuipanua barabara ya Rangi tatu hadi Mwarusembe iwe ya njia nne na kuwa atahimiza ujenzi wa kituo cha mabasi cha Kipala mpakani huku akiiagiza TARURA kuhakikisha kuwa barabara zilizo chini ya uangalizi wake zinapitika wakati wote wa mwaka na baadae ziingizwe kwenye mpango wa kuwekewa lami.
Juu ya ombi la bandari yaKisiju, Waziri Mkuu alieleza kuwa atalifikisha hilo kwa Rais na akaelekeza Mkuu wa Wilaya, Mkurugenzi na madiwani wa Mkuranga kuondoa changamoto ya abiria kutoshushwa eneo la mti pesa.
Akiongelea mtandao wa umeme, Waziri Mkuu alieleza kuwa lengo ni vijiji vyote 125 vya Wilaya ya Mkuranga viwe na umeme na kwamba bei ya kuunganisha majumbani huko vijijini ni sh. 27,000,00.
Ili kuondoa changamoto ya migogoro ya ardhi, Waziri Mkuu aliwaasa wananchi kutenga ardhi kwa matumizi mbalimbali ikiwa ni pamoja na maeneo ya ujenzi wa viwanda na kuwa wasiuze ardhi ovyo na akaielekeza halmashauri kupima maeneo ili wananchi wapate hati.
Mhe. Majaliwa pia alitoa rai kwa viwanda vyote kutoa ajira kwa vijana wa maeneo vilipo viwanda hivyo.
Nae Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhe. Abubakar Kunenge amemshukuru na kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwatumikia wananchi na kuwaletea maendeleo.
Mhe. Kunenge ametoa shukrani na pongezi hizo leo Novemba 27, 2022 wakati wa kumkaribisha Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa kuzungumza na wananchi wa Mkuranga.
Katika shukrani na pongezi zake, Mhe. Kunenge alibainisha kuwa inatokana na kazi kubwa anazozifanya Mhe. Samia za kuboresha hali ya wananchi wa Mkoa wa Pwani kimaendeleo na huku akitaja kuwa Mkoa wake umepewa kiasi cha sh. na sh. 6,820,000,000.00 za ujenzi wa madarasa 341 ya sekondari tayari kwa mapokezi ya wanafunzi wa kidato cha kwanza kuanza masomo Januari 2023.
Kwa uapande wake Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Mkuranga Mhe. Abdallah Ulega aliwasilisha maombi mbalimbali ikiwa ni pamoja na la ujenzi wa hospitali mpya ya Wilaya, ujenzi wa kituo cha magari ya abiria (stendi ya mabasi) Kipala mpanai na Ujenzi wa barabara ya Mkuranga hadi Kisiju ambako kuna bandari ya historia.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.