Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa kibali cha kuajiri watumishi elfu 13 katika sekta ya afya ili wapangiwe kufanya kazi kwenye vituo vya kutolea huduma hiyo kote nchini.
Hayo yamebainishwa leo Novemba 30, 2023 na Waziri wa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa - TAMISEMI ambaye ni Mbunge wa Rufiji Mohamed Mchengerwa wakati akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya chama cha Mapinduzi - CCM mbele ya viongozi wa chama hicho na wananchi kwenye viwanja vya Ujamaa Ikwiriri, Rufiji.
"Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ameendelea kuto ajira kwenye sekta ya afya na Rufiji imeendelea kupokea maafisa afya katika maeneno mbalimbali na hivi karibuni ameshatoa kibali cha kuajiri maafaisa afya, waganga (madaktari) takribani elfu 13, watakapoajiriwa, watapangiwa kazi kwenye vituo vyote vilivyojengwa wakati wa awamu ya sita kote nchini" amesema.
Mchengerwa ametoa taarifa ya kibali hicho cha Rais alipokuwa akifafanua maendeleo ya sekta ya afya kwenye Jimbo lake la Rufiji ambapo amesema kuwa katika kipindi cha 2021 hadi 2023 vituo vya afya vimeongezeka kutoka vinne hadi sita, Zahanati zimeongezeka kutoka 23 hadi 30 na akaongeza kuwa pamoja na mambo mengine, wamekamilisha ujenzi wa Jengo la Wagonjwa wa Dharura ikiwa ni pamoja na kukamilisha ujenzi wa jengo la Mionzi katika Hospitali ya Wilaya na vyote hivyo tayari vimeanza kutoa huduma kwa wana Rufiji.
"Tunaishukuru Serikali, kwani katika kipindi cha kuanzia Mwezi Julai, 2023 hadi Oktoba, 2023 tayari Sekta ya Afya imepokea jumla ya Shilingi 1,438,848,000.00 ambazo zimeanza kutekeleza miradi ya Ukarabati wa Miundombinu ya Hospitali ya Wilaya, Ukamilishaji wa Zahanati na Ujenzi wa Zahanati Mpya, Ujenzi wa Matundu ya vyoo na Miundombinu yake na Ukamilishaji wa Jengo la Wodi ya Wazazi, ameeleza.
Mchengerwa ameongeza kuwa vifaa tiba vimepelekwa katika vituo vyote vya afya na kuwa pamoja na uwepo wa Hospitali ya wilaya, kiasi cha sh. Bil. 10 kimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa hospitali ya kisasa itakayotoa huduma za kupokea na kuhudumia wagonjwa watakaokuwa wakipata rufaa kutoka kwenye vituo vingine vya afya wilayani humo.
Mchengerwa pia ameongelea maendeleo katika sekta za elimu, maji, miundombinu, kilimo na huduma za kijamii, uwezeshaji wananchi kiuchumi ikiwa ni pamoja na ujenzi wa masoko ya kisasa na maeneo mengine mbalimbali.
"Sisi Rufiji tunakiri kabisa, katika mambo ambayo tulilazimika kuyafanya makubwa ni kuwaahidi watanzania wa Rufiji kwamba tunaweza kubadilisha maisha yao katika mambo yanayowakera, tulipata tabu kwa miaka mingi ya nyuma katika sekta mbalimbali, sikuwa na sababu kwanini nisifanye kazi usiku na mchana kubadilisha maisha yao, watanzania wa Rufiji kwa miaka mingi wametamani maendeleo," amesema.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.