Serikali ya Cuba imeahidi kuendeleza na kuongeza ushirikiano wake na Mkoa wa Pwani, pamoja na Tanzania kwa ujumla, hususan katika sekta za afya na kilimo kupitia utoaji wa wataalam kutoka Cuba.
Hayo yameelezwa , Novemba 25, 2025, na Balozi wa Cuba nchini Tanzania, Yordenis Vera, alipotembelea Mkoa wa Pwani katika ziara maalum ya kuenzi kumbukizi ya miaka tisa tangu kufariki kwa aliyekuwa Rais wa Cuba, Fidel Castro, na kutambua mchango wake katika kuimarisha uhusiano na aliyekuwa Rais wa Kwanza wa Tanzania, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Ziara hiyo inalenga kuendeleza misingi ya ushirikiano iliyowekwa na viongozi hao wawili.
Akizungumza wakati wa mazungumzo hayo, Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge, alisema mkoa huo una mazingira rafiki kwa uwekezaji kutokana na uwepo wa miundombinu muhimu ikiwemo reli ya kisasa, bandari kavu ya Kwala, bandari ya Bagamoyo, barabara za kisasa, umeme wa uhakika, gesi, pamoja na upatikanaji wa maji ya kutosha.
Kunenge alimhakikishia Balozi Vera kuwa Serikali ya Mkoa itaendelea kushirikiana na Cuba katika kuongeza fursa za maendeleo kwa wananchi na kuimarisha sekta zinazobeba uchumi wa mkoa.
Uhusiano kati ya Tanzania na Cuba umeendelea kuwa imara kwa miaka mingi, ambapo Cuba imekuwa mshirika muhimu katika sekta ya elimu, na afya ikionyesha mfano kupitia ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Wasichana Ruvu na Shule ya Sekondari ya Kibiti.
Katika ziara hiyo, Balozi Vera alipokea taarifa kuhusu maendeleo ya Mkoa wa Pwani pamoja na fursa za uwekezaji zilizopo, na baadaye kutembelea Shule ya Sekondari ya Wasichana Ruvu
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.