Serikali imeiagiza Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba TMDA na Bohari kuu ya Dawa MSD, kufanya ukaguzi katika kiwanda cha kuzalisha vitendanishi kwa ajili ya kupima sampuli za damu kilichopo Halmashauri ya Mji wa Kibaha mkoani Pwani ili kianze uzalishaji.
Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Godwin Mollel amezindua kiwanda hicho kijulikanacho kwa jina la Action Medeor kilichopo Kibaha mkoani Pwani na akasema kiwanda hicho kitapunguza gharama za ununuzi wa vitendanishi walizokuwa wakinunua kwa shilingi 300,000 hadi 400,000 na sasa uwepo wa kiwanda hicho utapunguza gharama hizo hadi sh. 80,000.
Kutokana na hilo amemuagiza Mkurugenzi wa TMDA na MSD kufika kiwandani hapo ndani ya wiki mbili ili kukagua na kutoa kibali cha kuanza uzalishaji wa vitendanishi.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Afya Zanzibar, Hassan Hafidh amesema umefika wakati kwa serikali kuyafuta makampuni ambayo yanauza bidhaa hiyo kwa gharama kubwa zinazowashinda wananchi kumudu.
“Nimefurahishwa na uwekezaji mkubwa wa kiwanda hiki na niseme tu kuwa gharama za bidhaa hii kiwandani hapa wanauza kwa bei rafiki kabisa, sasa nakwenda Zanzibar nitafuta viwanda vyote vinavyouza vitendanishi kwa gharama kubwa,” amesema Naibu Waziri Hafidh.
Nae Mkurugenzi Mtendaji wa kiwanda cha Actiob Medeor, Christoph Bonsmann, amesema kiwanda hicho kitapunguza gharama za matibabu nchini Tanzania kwa zaidi ya asilimia 200.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge, Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Nickson Saimon amesema uwepo wa kiwanda hicho utaipunguzia mzigo serikali katika uendeshaji wa shughuli zake za matibabu.
Amesema serikali inatumia gharama kubwa katika kuhakikisha huduma za matibabu nchini zinapatikana kwa urahisi hivyo uwepo wa kiwanda hicho ni sehemu ya kuunga mkono jitihada hizo na kwamba wanafurahi mkoa wa Pwani kuwa sehemu ya uwekezaji wa huduma za matibabu.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.