Serikali imeiagiza, Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Bagamoyo, kukifuta kitongoji cha Kajanjo chenye makazi 120 ya makambi ya wavuvi ndani ya hifadhi ya mikoko Saadani.
Agizo hilo limetolewa Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge Juni 6, 2023 na kwenye mkutano wa hadhara na wananchi wa Kijiji cha Saadan, kata ya Mkange iliyopo wilayani Bagamoyo Mkoa wa Pwani na akaelekeza kuwa utekelezaji wa wakazi hao kuondoka kwenye eneo hilo ufanyike na kitongoji hicho kufutwa mara moja.
Amesema agizo hilo ni utekelezaji wa maamuzi ya baraza la mawaziri kufuatia ushauri wa timu ya Mawaziri wanane wa kisekta pamoja na timu ya wataalam iliyoundwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kushughulikia migororo yote ya ardhi nchini ikiwamo na Mkoa wa Pwani.
Amesema kuwa baada ya kufanyika tathmini ya mgogoro wa ardhi katika hifadhi ya Taifa ya Saadan (SANAPA), Serikali imeelekeza wananchi wote waliovamia eneo la mikoko kuondoka mara moja.
Aidha ameamuagiza Kamishna Msaidizi wa Ardhi kufuta hati ya upimaji wa kiwanja namba 2. sehemu ya Uvinje, Saadan yenye ukubwa wa eneo la ekari 19.42 yenye usajili namba 47522.
Amesema sababu ya kufuta kwa hati hiyo ni kuwa vipo ndani ya mipaka ya hifadhi na havina maendelezo yaliyokusudiwa baada ya kuuziana kati ya mmiliki Chuma Bakari kwenda kwa mmiliki wa sasa East African Resorts Limited.
“TFS na Mkurugenzi wa Halmashauri nawaagiza mfute makazi ya 120 ya makambi ya uvuvi, yaondolewe ndani ya hifadhi ya mikoko na kitongoji hiki cha Kajanjo kifutwe, aidha namuagiza Kamishna Msaidizi wa Ardhi na Mkurugenzi mfute leseni ya kampuni ya Sea Salt na ipunguzwe ili kuondoa eneo la ekari 50 ambalo litamegwa na kupewa wananchi wa Uvinje wanaohamishwa kutoka kwenye hifadhi ya Mikoko,” amesema Kunenge.
Aidha, Kunenge ameitaka Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania TFS, kuhakikisha inasimamia mapato yatokanayo na matumizi ya Malikale zilizopo ndani ya eneo la hifadhi ikiwemo majengo yanayotumika kama vile ya hoteli pamoja na nyumba za kulala wageni.
“Maagizo haya ni sehemu ya utekelezaji wa ilani ya Chama cha Mapinduzi CCM katika kuwatumikia wananchi kwa kuhakikisha migororo ya ardhi inatatuliwa kwa kuzingatia utawala wa sheria na kwa mujibu wa sheria ya nchi Rais ndiye msimamizi wa ardhi yote nchini kwa niaba yetu,” amesema Kunenge.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.