Serikali kupitia mpango wa TACTIC imetoa kiasi cha shilingi bilioni 19.8 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mitatu mikubwa katika Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha, mkoani Pwani. Miradi hiyo inahusisha ujenzi wa soko la kisasa la Mnarani na barabara mbili zenye urefu wa jumla ya kilomita 4.8.
Barabara zitakazojengwa kupitia mpango huo ni barabara ya Tughe–Anglican yenye urefu wa km 1.1, pamoja na barabara ya Picha ya Ndege–Hospitali ya Lulanzi–NDC yenye urefu wa km 3.7.
Mkataba wa utekelezaji wa miradi hiyo umesainiwa leo Septemba 25, 2025 baina ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Kibaha, Dkt. Rogers Shemgelekw na Mkandarasi M/s Dimetoclasa Real Hope Limited, katika hafla iliyoshuhudiwa na Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhe. Abubakar Kunenge.
Akizungumza mara baada ya tukio hilo, Mhe. Kunenge alisema serikali inaleta miradi hiyo muhimu kwa wananchi wa Kibaha kwa lengo la kuboresha utoaji wa huduma na kuinua hali ya uchumi wa wananchi, hasa wenye kipato cha chini.
“Tunafahamu kuwa wananchi wanahitaji huduma bora katika masoko, na ndiyo maana serikali imeanzisha mradi huu. Lengo ni kuhakikisha wananchi wanapata mazingira mazuri ya kufanyia biashara kwa ubora unaostahili,” alisema RC Kunenge.
Aidha, aliwataka wafanyabiashara watakaotumia soko hilo kushiriki katika kugharamia uendeshaji wake, akisisitiza kuwa fedha zilizotumika ni mkopo kutoka Benki ya Dunia, hivyo zinapaswa kurejeshwa.
“Ni lazima tutafute utaratibu mzuri wa kuchangia gharama za uendeshaji wa soko hili. Kama mnavyofahamu, hizi ni fedha za mkopo ambazo tunapaswa kuzirejesha,” alieleza Kunenge.
Mkuu huyo wa mkoa alisisitiza kuwa hadhi ya Manispaa ya Kibaha inapaswa kuendana na huduma zinazotolewa kwa wananchi, hivyo miradi hiyo ni sehemu ya kuboresha taswira ya mji na maisha ya wananchi.
Katika hatua nyingine, Mhe. Kunenge alimuelekeza mkandarasi wa mradi huo kuhakikisha utekelezaji unafanyika kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa.
“Nafahamu uwezo wenu uko vizuri. Mmehakikishiwa kuwa fedha zipo, hivyo sitarajii kuona changamoto yoyote. Ninataka mradi huu ukamilike ndani ya muda uliopangwa kama ilivyoelekezwa kwenye mkataba,” alisema.
Naye Katibu Tawala Mkoa wa Pwani Pili Mnyema ameshukuru serikali kwa mradi huo mkubwa na kuahidi kusimamia kwa weredi na kuhakikisha unakamilika kwa wakati.
Kwa upande wake, Mhandisi Emmanuel Manyanga, Mratibu Msaidizi wa Mradi wa TACTIC, alisema kuwa lengo kuu la mradi huo ni kuboresha usimamizi wa ukuaji wa miji na kuwezesha Halmashauri kutoa huduma bora na endelevu kwa wananchi.
Alifafanua kuwa kazi zitakazofanyika kupitia mkataba huo ni pamoja na Ujenzi wa barabara ya Tughe–Anglican (km 1.1), Ujenzi wa barabara ya Picha ya Ndege–Hospitali ya Lulanzi–NDC (km 3.7), Ujenzi wa soko la kisasa la Mnarani, Uboreshaji wa bustani ya mapumziko ya mji.
Utekelezaji wa mkataba huo unatarajiwa kuanza rasmi Oktoba 1, 2025 na kukamilika Desemba 12, 2026.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.