Huduma ya afya inazidi kuimarika wilayani Kibiti, Mkoani Pwani baada ya Serikali kufanya upanuzi wa huduma katika hospitali ya wilaya kwa kuongeza majengo makubwa manne ya upasuaji, wodi ya wanaume na ya wanawake, wagonjwa pamoja na jengo la kuhifadhia maiti.
Akitembelea na Kuweka Jiwe la Msingi katika majengo hayo, Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Godfrey Mzava ameiagiza Halmashauri ya Kibiti kutekeleza kwa haraka maalekezo aliyoyatoa ili majengo yaanze kutoa huduma iliyokusudiwa.
"Mradi huu ni mradi muhimu, umegharimu milioni 800 kutoka Serikali Kuu kwa ajili ya wodi ya upasuaji na kuhifadhia maiti"
Nao baadhi ya wakazi wa Kibiti, akiwemo Amina Saidi na Zuena Amir wameeleza faraja yao kwani upatikanaji wa huduma muhimu zitapatikana kwa karibu.
Aidha Mwenge ukipitia mradi wa maji kijiji cha Mjawa, uliogharimu kiasi cha sh.milioni 503.6 na kusimamiwa na RUWASA, Mzava alitoa rai kwa wananchi kuulinda na kuutunza kwa manufaa ya kudumu muda mrefu.
Hata hivyo amesisitiza umuhimu wa manunuzi ya umma kutumia mfumo wa kidigital wa manunuzi ya umma Nest ambao unasimamiwa na mamlaka ya udhibiti ya manunuzi ya umma (PPRA).
Alieleza mfumo huo, unasaidia kuondoa tabia iliyokuwa ikijitokeza kipindi cha mfumo wa zamani TANREP.
Mzava alifafanua, mfumo huo umeondoa malalamiko,na tabia za watu kukutana mezani na kupeana zabuni.
Kaimu Meneja wa RUWASA Kibiti, Juma Ndaro alisema, Mradi wa maji Mjawa utahudumia wananchi wa kijiji hicho wapatao 3,113 na umefikia asilimia 80.
Mwenge wa Uhuru ulipokelewa Wilayani Kibiti ukitokea wilaya ya Rufiji Mei 6, 2024, ambapo Mkuu wa wilaya ya Kibiti Kanal Samwel Kolombo ameeleza, umepitia miradi 15 yenye thamani ya sh.bilioni 2.4.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.