Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU), Mhe. Dkt. Tulia Ackson, amesisitiza umuhimu wa kuuenzi na kuulinda Muungano wa Tanzania, akisema kuwa Muungano huo ni kichocheo kikubwa cha maendeleo ya kiuchumi, kisiasa, kijamii na kitamaduni kwa Taifa.
Akizungumza leo na wananchi wa Mkoa wa Pwani katika ziara yake ya siku moja, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Miaka 61 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar yaliyofanyika Kibaha Shopping Mall, Dkt. Tulia alisema Muungano umejenga msingi wa mshikamano na umoja miongoni mwa Watanzania.
“Tanzania inaendelea kuwa kisima cha amani na inatambulika dunia nzima. Muungano huu umechangia kwa kiasi kikubwa kutufanya tuwe na sauti moja na kutambulika kimataifa. Umenisaidia hata mimi kuweza kushika nafasi ya Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani,” alieleza Mhe. Dkt. Tulia.
Alisisitiza kuwa ingawa vijana wengi hawakushuhudia kuasisiwa kwa Muungano huo, ni wajibu wao kuuenzi na kuudumisha kwa kuzingatia matendo na maneno yanayoujenga na kuulinda.
“Watanzania tuulinde Muungano kama vile waasisi wetu walivyofanya. Vijana kama sisi hatukuwepo enzi hizo, lakini Muungano tumeukuta na tunaendelea kuudumisha. Niwasihi tufakari matendo na maneno yetu ili yawe na mchango chanya kwa Muungano wetu,” alisisitiza.
Katika hotuba yake, Dkt. Tulia pia alizungumzia maboresho ya sheria ya ukaguzi yaliyofanywa kwa kuzingatia maoni ya wananchi na wadau, akieleza kuwa mabadiliko hayo yamechochewa na falsafa ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kupitia dhana ya “4R” (Reconciliation, Resilience, Reforms, Rebuilding).
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Mhe. Ridhiwani Jakaya Kikwete, alieleza kuwa Muungano umekuwa chachu ya maendeleo, hasa katika kudumisha mahusiano mazuri baina ya Tanganyika na Zanzibar ambayo yamechangia kwa kiasi kikubwa ustawi wa Mkoa wa Pwani.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhe. Abubakar Kunenge, alieleza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia imewekeza zaidi ya shilingi trilioni moja kwa ajili ya miradi ya maendeleo katika mkoa huo. Alisema mkoa huo umekamilisha jumla ya viwanda vikubwa 78, na kufikisha idadi ya viwanda 1,553, vikiwemo 128 vikubwa.
“Yeyote anayetaka kuthibitisha utumishi uliotukuka wa Mhe. Rais aje Mkoa wa Pwani. Pwani imefunguka kwa juhudi za Mhe. Rais, na pia amekuwa mfano bora kwa watoto wa kike katika kufanya vizuri mashuleni,” alisema Mhe. Kunenge.
Kaulimbiu ya maadhimisho ya miaka 61 ya Muungano mwaka huu ni: “Muungano Wetu ni Dhamana, Heshima na Tunu ya Taifa – Shiriki Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025.”
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.